Muigizaji maarufu ashtakiwa kwa kushindwa kulipa bili ya baa ya Sh150,000

Muhtasari

•Muigizaji huyo aliagiza vipande viwili vya kuku yenye thamani ya Sh3,000, kinywaji kimoja cha cocktail chenye thamani ya Sh2,000, chupa mbili za 300ml za soda zenye thamani ya Sh500.

•Hakimu alikubali na kumwachilia kwa bondi ya Sh100,000 kwa dhamana mbadala ya pesa taslimu Sh50,000.

Dorah Clara Ojenge katika mahakama ya Kibera
Dorah Clara Ojenge katika mahakama ya Kibera
Image: CLAUSE MASIKA

Muigizaji maarufu nchini Kenya ameshtakiwa kwa kushindwa kulipa bili ya Sh152,550  baada ya kula na kunywa pombe ya bei ghali katika mkahawa wa jijini.

Dorah Ojenge almaarufu Mishi Dorah alishtakiwa katika Mahakama ya Kibera siku ya Ijumaa ambapo alikanusha mashtaka.

Kulingana na mahakama, alikuwa katika baa hiyo mnamo Mei 26 na Mei 27.

Kisha aliagiza vipande viwili vya kuku yenye thamani ya Sh3,000, kinywaji kimoja cha cocktail chenye thamani ya Sh2,000, chupa mbili za 300ml za soda zenye thamani ya Sh500.

Pia aliagiza chupa ya lita moja ya maji yenye thamani ya Sh400 na chupa tatu za kinywaji cha Red Bull zenye thamani ya Sh1,650.

Mahakama pia ilisikiza kwamba muigizaji huyo anadaiwa kuagiza chupa sita za Belaire Luxe (750ml) zenye thamani ya Sh75,000 na chupa saba za Hennessy VS (750ml) za thamani ya Sh70,000 ambazo alizifurahia na kundi la marafiki.

Alipotakiwa kulipa, Ojenge alisemaakaunti yake ya  benki ilikuwa na matatizo na ilishindwa kulipa.

Dora hata hivyo alikanusha mashtaka yote dhidi yake mbele ya hakimu mkuu mwandamizi wa Kibera Monica Maroro.

Wakili wake Mwihaki Nganga aliambia mahakama kuwa mwigizaji huyo hawezi kutoweka  na anafaa kuachiliwa kwa dhamana.

"Heshima yako, mteja wangu sio hatari ya kukimbia na hatakosa kufika  mahakamani," Nganga alisema.

Hakimu alikubali na kumwachilia kwa bondi ya Sh100,000 kwa dhamana mbadala ya pesa taslimu Sh50,000.

Kesi hiyo itatajwa mnamo Juni 16.