Jamaa aliyepatikana uchi nyumbani kwa mwanamke mzee atuhumiwa kwa ubakaji

Mwanaume huyo alifumaniwa juu ya ajuza huyo akiwa uchi wa mnyama.

Muhtasari

•Mahakama ilisikia kwamba mshtakiwa alitenda kosa hilo mnamo Agosti 27 katika Uwanja wa Ndege wa Wilson bila ridhaa ya mwathiriwa.

•Mshtakiwa alikana kutenda kosa lolote na akaomba masharti nafuu ya bondi.

Picha ya Kitanda
Image: BBC

Mwanamume mmoja aliyepatikana akiwa uchi katika nyumba ambapo mwanamke mzee alikuwa akistarehe alishtakiwa kwa kujaribu kumbaka.

Jamaa huyo pia alishtakiwa kwa kosa lingine la kufanya kitendo kichafu na mtu mzima kinyume na Sheria ya Makosa ya Kujamiiana.

Alikanusha mashtaka hayo mbele ya hakimu mkuu mwandamizi wa Kibera, Esther Boke.

Mahakama ilisikia kwamba mshtakiwa alitenda kosa hilo mnamo Agosti 27 katika Uwanja wa Ndege wa Wilson bila ridhaa ya mwathiriwa.

Kulingana na karatasi za mahakama, wanaume wawili walikuwa wamemtembelea mwathiriwa nyumbani kwake walipomfumania mshtakiwa akiwa juu ya mwanamke huyo huku akiwa uchi wa mnyama.

Walimkamata na kumpeleka katika kambi ya chifu wa Uwanja wa Ndege wa Wilson lakini si kabla ya umati kumpiga kitutu nje ya nyumba.

Mahakama ilisikia kuwa wakiwa katika kambi ya chifu, walishauriwa kumpeleka mshtakiwa katika kituo cha polisi cha Akilla.

Baadaye walirudi nyumbani pamoja na polisi kujaribu kumpeleka mwathiriwa hospitalini kwa uchunguzi wa kimatibabu lakini walimkuta akiwa na vurugu.

Waliondoka nyumbani na baada ya saa kadhaa walirudi na kumpeleka Nairobi Women Hospital baada ya kufanikiwa kumshawishi.

Karatasi za mahakama zinasema kuwa hakuna ushahidi juu ya ubakaji uliopatikana wakati wa uchunguzi wa matibabu.

Mshtakiwa alikana kutenda kosa lolote na akaomba masharti nafuu ya bondi.

Mahakama ilimwachilia kwa bondi ya Sh500, 000 bila dhamana ya pesa taslimu.

Kesi hiyo itatajwa Septemba 13.