Mwanamke ashtakiwa kwa kumtupa mtoto wake mchanga kwenye choo

Mshukiwa alikana mashtaka hayo alipofika mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Caroline Ateya.

Muhtasari

•Diana Muyanda anadaiwa kufanya kitendo hicho mnamo Januari 19 ambapo alitupa mtoto huyo mchanga chooni baada ya kujifungua na akaaga.

•Hakimu mkazi mkuu aliamuru mshtakiwa apelekwe hospitalini kwa uchunguzi wa kiakili na atazuiliwa katika kituo cha polisi cha Kabarnet hadi kesi itakapotajwa Januari 30.

ambapo mwanamke wa makamo alifikishwa mahakamani akidaiwa kumtupa mtoto wake mchanga mara baada ya kujifungua.
Bango la mahakama ya sheria ya Kabarnet ambapo mwanamke wa makamo alifikishwa mahakamani akidaiwa kumtupa mtoto wake mchanga mara baada ya kujifungua.
Image: Michelle Yatich

Mwanamke mwenye umri wa makamo alifikishwa katika mahakama ya Kabarnet siku ya Jumatatu akishtakiwa kwa mauaji ya mtoto mchanga baada ya kudaiwa kumtupa mtoto wake mchanga mara baada ya kujifungua.

anadaiwa kufanya kitendo hicho mnamo Januari 19, mwaka huu, majira ya saa mbili usiku katika lokesheni ya Marigat, eneo bunge la Baringo Kusini ambapo alitupa mtoto huyo mchanga chooni baada ya kujifungua na akaaga.

Mshukiwa alikana mashtaka hayo alipofika mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Caroline Ateya.

Wakili wa upande wa mashtaka Casmir Obiero aliomba korti kwamba mshtakiwa apelekwe kufanyiwa uchunguzi wa kiakili katika hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Baringo, Kabarnet, huku uchunguzi wa maiti ukifanywa kwa mtoto ili kubaini chanzo hasa cha kifo hicho.

Hakimu mkazi mkuu aliamuru mshtakiwa apelekwe hospitalini kwa uchunguzi wa kiakili na atazuiliwa katika kituo cha polisi cha Kabarnet hadi kesi itakapotajwa Januari 30.

Katika mahakama hiyo kijana mwenye umri wa miaka 22 alishtakiwa kwa jaribio la kufanya mapenzi na mwanafamilia kinyume na kifungu cha 20(2) cha Sheria ya Makosa ya Kujamiiana Na.3 ya mwaka 2006.

Kwa mujibu wa shtaka hilo, Franklin Komen anadaiwa kuwa mnamo Januari 3, mwaka huu, majira ya saa tatu usiku katika kijiji cha Barketiew, eneo la Kapkata katika Kaunti ndogo ya Baringo Kaskazini, kwa makusudi na isivyo halali alidai kufanya mapenzi na binamu yake mwenye umri wa miaka 16.

Akisomewa mashtaka yanayomkabili mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Caroline Ateya, mshtakiwa alikana kutenda kosa hilo.

Hakimu alimwachilia kwa bondi ya Sh 100,000 na mdhamini mmoja wa kiasi sawa na hicho.

Ateya aliagiza kesi hiyo isikizwe Machi 7 ambapo mashahidi wanne watakapangwa kutoa ushahidi kuthibitisha kesi hiyo.