Korti yataka DNA kufanywa baada ya mama kupokezwa mtoto aliyekufa, jinsia tofauti

Mama alisema alijifunga mtoto wa kiume lakini baadae akaambiwa ni wa kike ambaye pia alitaarifiwa amefariki dunia.

Muhtasari

• Hakimu aliruhusu amri hizi, akifungua mlango wa kupima DNA ili kubaini ukweli.

• Baada ya kujifungua, aliambiwa mtoto alikuwa na matatizo na kuhamishiwa hospitali nyingine.

• Kufika hospitali ya pili, akitaka kuona mtoto wake akaambiwa ni wa kike wakati yeye alijifungua wa kiume.

• Huyo wa kike, aliambiwa pia alikuwa amekata kamba.

Kifaa cha kupima DNA nyumbani
Kifaa cha kupima DNA nyumbani
Image: Maktaba

Mahakama ya Mombasa imeamuru uchunguzi wa DNA kufanyiwa mwili wa mtoto mchanga baada ya mama kudai mtoto huyo si wake.

Inaarifiwa kwamba mama huyo alielekea katika hospitali moja kaunti ya Mombasa na kujifungua mtoto aliyesema ni wa kiume.

Lakini baada ya kujifungua, madaktari walibaini kwamba mtoto huyo hakuwa na kilo za kutosha ambapo alihitajika kupewa huduma maalum ambayo kwa bahati mbaya haikuwa inapatikana katika hospitali hiyo.

Hapi ndipo walimchukua mtoto yule kwa hospitali nyingine – Coast General ambapo huduma hiyo ilikuwa inapatikana.

Baadae mama yule pia alipelekwa katika hospitali hiyo akihamishwa kutoka ile ya kwanza, na alipofika alitaka kuona mtoto wake.

Hapo ndipo kizaazaa kilianza baada ya kuambiwa kwamba mtoto wake alikuwa wa kike wakati yeye anashikilia kwamba alijifungua mtoto wa kiume katika hospitali ya kwanza.

Alisisitiza kutaka kumuona mtoto wake na ndipo akaambiwa kwamba mtoto wake ambaye ni wa kike sasa alikuwa amefariki na mwili wake ulikuwa umehifadhiwa katika chumba cha makafani cha hospitali hiyo ya pili.

Mume wake alifika pia na wote wakakataa kuwa mtoto huyo si wao, wakisisitiza kwamba mtoto wao alikuwa wa kiume, jambo lililowapelekea kuhusisha taasisi za kisheria ili kupata kile ambacho walitaja kuwa haki.

Jambo hilo lilifikishwa katika mahakama ya Mombasa ambapo wapelelezi wa jinai ukanda wa pwani waliiambia mahakama;

“Wazazi wa watoto wachanga katika kesi hii wamezozana mtoto aliyekufa aliyewasilishwa kwao katika hospitali ya Coast General Teaching and Referral.”

DCI iliitaka mahakama kukubali ombi la DNA kwa chembechembe hizo za watoto hao ili kubaini ikiwa ni kweli mtoto ni wa wanandoa hao au wako sahihi kupinga.

Hakimu aliruhusu amri hizi, akifungua mlango wa kupima DNA ili kubaini ukweli.