Seremala afungwa miaka 45 jela kwa kumuua mwanafunzi aliyemkataa baada ya kumtongoza

Mfungwa huyo anasemekana kumpiga mwanafunzi huyo aliyefariki kutokana na majeraha ya kitu butu kichwani kisha kumbaka kabla ya kumkata miguu baada ya kukataa matamanio yake ya ngono.

Muhtasari

• Akitoa hukumu hiyo, Hakimu Reuben Nyakundi alitaja jinsi mshtakiwa alivyomuua Emmah Wanyota kuwa ya kinyama na ya kikatili.

Mahakama ya mjini Eldoret hatimaye imekamilisha kesi ya mauaji ya mwanafunzi wa kozi ya urembo aliyeuawa na seremala mwaka 2019 baada ya kumkataa kimapenzi.

Emma Wanyota, mwanafunzi wa Vera Beauty College aliuawa kikatili na mshukiwa Mustafa Idd ambaye sasa amepatikana na hatia ya kutekeleza mauaji hayo na kuhukumiwa kifungo cha miaka 45 jela.

Akitoa hukumu hiyo, Hakimu Reuben Nyakundi alitaja jinsi mshtakiwa alivyomuua Emmah Wanyota kuwa ya kinyama na ya kikatili.

Idd anashtakiwa kwa kumuua aliyekuwa mwanafunzi wa chuo cha urembo cha Vera chenye makao yake mjini Eldoret mnamo Septemba 30, 2019 nyumbani kwa mzazi wake huko Moi’s Bridge, Kaunti ya Uasin Gishu.

Chumba cha mahakama kilizingirwa na wanafamilia wa mwanafunzi aliyeuawa wakiongozwa na mamake Beatrice Wanyota na dadake pacha Sharon mapema saa 8:30 asubuhi.

Kulikuwa na hali ya taharuki mahakamani pale mama wa marehemu alipoangua kilio wakati Hakimu alipokuwa akitoa hukumu dhidi ya mfungwa huyo na kumlazimisha msaidizi wa hakimu kumpoza.

Jaji Nyakundi alibainisha jinsi marehemu alivyoteswa na kusababisha mauaji yake ya kikatili katika siku ya maafa.

Mfungwa huyo anasemekana kumpiga mwanafunzi huyo aliyefariki kutokana na majeraha ya kitu butu kichwani kisha kumbaka kabla ya kumkata miguu baada ya kukataa matamanio yake ya ngono.

Wakati wa kutoa ushahidi wake mahakamani hapo, mama wa marehemu Emmah alisimulia jinsi alivyomuacha bintiye ndani ya nyumba na kwamba aliporudi alikuta sebule yake ikiwa imetapakaa damu.

Alisema kuwa bintiye marehemu alikuwa amebakiwa na mwezi mmoja tu kumaliza masomo yake ya chuo kikuu.

Kulingana na dadake pacha wa mwanafunzi aliyeuawa, mwanamume huyo, ambaye ni seremala maarufu katika Moi’s Bridge Town, alikuwa mpenzi wa zamani wa marehemu.