Joseph 'Jowie' Irungu Kuhukumiwa Kwa Mauaji ya Monica Kimani

Mahakama iliamua kwamba upande wa mashtaka ulitoa ushahidi wa kutosha na kuthibitisha kuwa Jowie alimuua Monica.

Muhtasari

• Mwanahabari Jacque Maribe, ambaye alishtakiwa pamoja na Irungu, hata hivyo aliondolewa mashtaka ya mauaji.

, mshtakiwa wa kwanza katika mauaji ya mfanyabiashara Monica Kimani, katika Mahakama ya Milimani mnamo Februari 9, 2024. Picha: DOUGLAS OKIDDY
Joseph Irungu Jowie , mshtakiwa wa kwanza katika mauaji ya mfanyabiashara Monica Kimani, katika Mahakama ya Milimani mnamo Februari 9, 2024. Picha: DOUGLAS OKIDDY

Joseph Irungu, almaarufu 'Jowie', ambaye alishtakiwa kwa mauaji ya mfanyabiashara Mkenya Monica Kimani, atajua hatima yake Ijumaa, Machi 8.

Hii ni baada ya kupatikana na hatia ya mauaji katika uamuzi uliotolewa na Jaji Grace Nzioka mnamo Februari 9, na kuhitimisha kesi ya mauaji iliyoanza mwaka wa 2018.

Mahakama ya Nairobi iliamua kwamba upande wa mashtaka ulitoa ushahidi wa kutosha na kuthibitisha bila shaka kwamba Jowie alimuua Monica.

Mwanahabari Jacque Maribe, ambaye alishtakiwa pamoja na Irungu, hata hivyo aliondolewa mashtaka ya mauaji, huku hakimu akisema kuwa shtaka la mauaji sio shtaka sahihi ambalo upande wa mashtaka ungependekeza dhidi yake.

“Baada ya kuzingatia ushahidi uliotolewa upande wa mashtaka umetoa ushahidi wa kutosha na umedhihirisha kuwa mtuhumiwa alitekeleza mauaji,” Hakimu Grace Nzioka alisema katika uamuzi wake.

Katika kesi ya Maribe, hakimu aliamua kwamba ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka dhidi yake haukumweka katika nyumba ya marehemu usiku wa mauaji hatua iliyopelekea aondolewe mashtaka ya mauaji.   

Jaji huyo hata hivyo alisema kwamba Maribe alikosea kutoa taarifa za uongo kwa maafisa wa upelelezi. Kuhusiana na kosa hili, hakimu alisema kuwa ni jukumu la afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma kuamua ni hatua gani ichukuliwe dhidi yake.