Mchomelea vyuma ahukumiwa kifungo cha miaka 210 jela kwa wizi wa mabavu, ubakaji

Shilisia alipatikana na hatia ya zaidi ya mashtaka matano na mahakama ya Eldoret.

Muhtasari

•Hakimu  Naomi Wairimu aliamuru hukumu hiyo iende sambamba, kumaanisha kwamba mshtakiwa atatumikia kifungo cha miaka 50 jela.

•Shilisia alishtakiwa kando kwamba mnamo tarehe sawana mahali sawa, alimbaka Gladys Rotich baada ya kuiba Sh 6,000.

Mahakama
Mahakama
Image: MAHAKAMA

Mchomelea vyuma mwenye umri wa miaka 55 aliyeshtakiwa kwa wizi wa mabavu amehukumiwa kifungo cha miaka 210 jela baada ya kupatikana na hatia ya zaidi ya mashtaka matano na mahakama ya Eldoret.

Washtakiwa wenzake Humphrey Shilisia, miongoni mwao mkewe Amina Melisi na David Gazemba waliondolewa mashtaka ya wizi huo kwa kukosa ushahidi.

Hakimu Mkuu Mwandamizi wa Eldoret Naomi Wairimu aliamuru hukumu hiyo iende sambamba, kumaanisha kwamba mshtakiwa atatumikia kifungo cha miaka 50 jela.

Shtaka dhidi ya washtakiwa hao watatu lilisema kuwa mnamo Juni 20, 2020, katika mtaa wa Wales katika kaunti ndogo ya Kapseret, kaunti ya Uasin Gishu, wakiwa wamejihami kwa silaha hatari walimuibia Gladys Rotich Sh. 6,000.

Shilisia alishtakiwa kando kwamba mnamo tarehe sawana mahali sawa, alimbaka Gladys Rotich baada ya kuiba Sh 6,000 kutoka kwa simu yake ya rununu.

Watatu hao pia walishtakiwa kuwa mnamo tarehe na mahali sawa, walimnyang’anya Yulita Mitei mali ya thamani ya Sh. 19,300

Pia walishtakiwa kuwa mnamo siku hiyo na mahali sawa, walimwibia Moses Rotich Sh. 76, 800 huku wakitishia kutumia vurugu halisi dhidi yake.

Washtakiwa hao walidaiwa kuwa tarehe sawa na mahali hapo hapo walimnyang’anya Gilbert Murei Sh 4,800.

Akitoa ushahidi wake dhidi ya Humphrey Shilisia, mlalamikaji alisimulia jinsi wavamizi hao walivyovamia nyumba yao usiku wakiwa na tochi.

 Alisema mshtakiwa wa kwanza alituma Sh6,000 kutoka kwa simu yake na baada ya kuhamisha pesa kutoka kwa simu ya mumewe, alimwamuru aingie chini ya kitanda.

“Kisha akaniamuru nitoke naye huku akinicharaza panga shingoni na kunibaka. Baada ya uhalifu huo aliomba funguo za gari na nilipomwambia kuwa sijui kuendesha gari aliniruhusu kurudi nyumbani na kufunga mlango na kuondoka,” alisimulia mlalamishi.

Katika maelezo yake, mshtakiwa wa kwanza alisema kuwa mnamo tarehe 20 Julai 2020, aliamka na kwenda kwenye kazi yake ya kuchomelea na kwamba wakati akirudi, alisimama ili kuwekewa muziki kwenye USB yake.

Alisema kuwa maafisa wawili wa polisi kutoka kituo cha polisi cha Langas walimsimamisha njiani na alitii.

Kulingana na mfungwa, maafisa hao walimtaka awapeleke nyumbani kwake kufanya msako wa kutafuta bunduki na kwamba wakiwa ndani ya nyumba hiyo, walichukua radio, TV, na mtungi wa gesi kabla ya kumkamata mkewe.

Mshitakiwa wa pili katika utetezi wake, aliiambia mahakama kuwa anashitakiwa kwa kosa la unyang’anyi kwa kutumia nguvu baada ya kukataa kufuata maagizo ya askari anayemkamata ya kumhusisha mtu mwingine katika shauri hilo.

"Nilihusishwa na mashtaka ya wizi wa kutumia nguvu baada ya kukataa kumhusisha mtu mwingine na kosa hilo," alisema Gazemba.

Akitoa hukumu kwa mshitakiwa wa kwanza, Hakimu Mfawidhi alisema kuwa bila shaka mlalamikaji Gladys aliibiwa kama inavyodaiwa.

"Pia kutoka kwa ripoti ya daktari, inaonyesha kwamba mlalamikaji alibakwa," aliamuru Hakimu.