Ken Walibora: Ulilima, ukapanda na kupalilia mbegu nyingi katika uhai wako

Muhtasari

• Ahsante kwa dhahabu ya wino wa kalamu yako, ambao ulinichochea kuchakura umbuji! Mola azidi kukurehemu pema penye wema!

• Walibora aliaga dunia 10 April 2020 baada kuhusika katika ajali ya barabarani.

WALIBORA: Profesa Ken Walibora, alifariki alipogongwa na basi. Picha: MOSES MWANGI
WALIBORA: Profesa Ken Walibora, alifariki alipogongwa na basi. Picha: MOSES MWANGI

“Mtu hafunzwi umbuji, lakini anaweza akachochewa.” Ni kauli yake marehemu profesa Ken Walibora, nilipokutana naye mara ya kwanza, punde tu baada ya kupata nafasi katika shirika la utangazaji nchini Kenya-KBC, mwaka 2003. Aliponisikiza kwa mara ya kwanza nikisoma habari za radio KBC, aliniambia kuwa nina sauti imara.

Kauli yake iliamsha hamu yangu ya kumaliza kiu ya kusoma kazi zake. Mwaka 2006, maktaba ya Macmilan, ilizidisha mahusiano yangu na gwiji huyo ambaye ameacha alama ya lugha ya Kiswahili nchini na nje ya nchi.

Nilikabidhiwa mswada wake wa Ndoto ya Almasi, kuuhariri, kwa kuzingatia maudhui, wahusika, mtiririko wa vitushi, matumizi ya lugha, ubora wa kazi yenyewe pamoja na ufaafu wa kichwa cha kazi hiyo. Nilimshauri abadilishe kichwa cha kazi hiyo, lakini alishikilia kuwa Almasi alikuwa anawakilisha ndoto za wahusika wengi.

Aidha nilimshauri abadilishe mwisho wa kazi hiyo kwa kutoa matumaini, kwani Almasi hakutimiza ndoto yake ya kuwa mtangazaji, lakini alishikilia kuwa ndoto za watu wengi katika jamii huwa hazitimii kutokana na mazingira mabaya ambayo hayalei vipaji. Hapo nilifahamu kuwa alikuwa mtu mwenye msimamo thabiti, lakini msikivu.

Mwaka 2011, marehemu alinijumuisha kwenye mkusanyiko wa kazi yake nyingine Sina Zaidi-Mkusanyiko wa hadithi fupi kutoka kwa wandishi mbali mbali. Alifanya nikaamini kuwa, mtu yeyote kutoka pembe yoyote ya taifa angeandika na kusema lugha ya Kiswahili kwa mlahaka mkubwa.

Mwaka 2018 alinipigia simu kutoka Kitale, alipofahamu kuwa mswada wangu wa Makovu ya Uhai, ulikuwa umeteuliwa miongoni mwa tatu bora kuwania tuzo ya fasihi ya Kiswahili, barani Afrika ya Mabati Cornel.

Pamoja na kuwa ndovu kwenye uwanja huu, Ken alikuwa sisimizi yalipofikia masuala ya kusikiza hoja za watu walioonekana kuwa hawakuwa wa kufu yake katika bahari ya Kiswahili. Alimpa kila mmoja nafasi bila ya kujalli, tabaka, kabila wala jinsia. 

Niseme kuwa, “mbegu hufa ardhini, kabla ya kuchipuka na kua mmea. Lakini siku zote tumaini la mkulima huwa halifi, licha ya mbegu kunyong’onyea ardhini.

Kwa Marehemu Profesa Ken Walibora. Ulilima, ukapanda na kupalilia mbegu nyingi katika uhai wako kupitia wino wako. Moja ya mbegu hizo ni Kengeza la Jasiri.

Ahsante kwa dhahabu ya wino wa kalamu yako, ambao ulinichochea kuchakura umbuji! Mola azidi kukurehemu pema penye wema! Ninaamini kuwa malaika wanafurahia jinsi kalamu yako inavyoteleza kwa kina cha mawazo! Japo ulituacha, kazi zako zitadumu milele.

Walibora aliaga dunia 10 April 2020 baada kuhusika katika ajali ya barabarani.

 

Shisia Wasilwa -Mwanahabari/Mwandishi-Dunia Tambara Bovu, Makovu ya Uhai, Kengeza la Jasiri.

MHARIRI: DAVIS OJIAMBO