Mwalimu auawa kwa kukatwakatwa, moyo wake watolewa Nyamira

Baadhi ya sehemu za mwili wa Momanyi Obonyo pia zilikatwa katika tukio hilo la mauaji.

Muhtasari

•Uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa mzozo wa ardhi unaweza kuwa chanzo cha mauaji ya Obonyo.

•Polisi walisema bado hawajajua nia ya kutolewa kwa moyo wa marehemu lakini wanashuku ilikuwa mauaji ya kitambiko.

crime scene
crime scene

Mwalimu mmoja mstaafu ameuawa na watu wasiojulikana na moyo wake kutolewa katika kaunti ya Nyamira.

Polisi na mashahidi walisema baadhi ya sehemu za mwili wa Momanyi Obonyo pia zilikatwa katika mauaji hayo ya Jumatatu jioni.

Mwili huo ulipatikana kwenye lango la nyumba yake iliyo Borabu.

Polisi walitembelea eneo la tukio Jumanne na kurekodi taarifa.

Uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa mzozo wa ardhi unaweza kuwa chanzo cha mauaji ya Obonyo, ambaye alifariki akiwa na umri wa miaka 54.

Polisi walisema bado hawajajua nia ya kutolewa kwa moyo wa marehemu lakini wanashuku ilikuwa mauaji ya kitambiko. Bado hakuna aliyekamatwa.

Mwili wa marehemu ulipelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Gucha katika mji wa Keroka, ukisubiri uchunguzi wa maiti.

Polisi wanasema mauaji hayo yalifanyika saa chache baada ya miili miwili ya vijana kupatikana ikiwa imefungwa kwenye sandarusi katika kaunti ndogo ya Bonchari huko Kisii Jumatatu.

Wawili hao walikuwa wamefungwa kwenye mti kabla ya kuuawa. Waligunduliwa kwenye lango la shule ya Msingi ya Nyamokenye.

Inadaiwa wawili hao walinaswa wakivunja nyumba katika soko la karibu la Gesonso Jumapili usiku na kuuawa na kundi la watu.

Msemaji wa polisi Bruno Shioso alisema wana wasiwasi kuhusu ongezeko la visa vya mauaji ya watu. Alisema polisi wataanzisha programu za kuelimisha watu kuhusu hatari zao.

"Watakaopatikana na masuala kama haya watashughulikiwa ipasavyo," alisema.

Wakati huo huo, wanaume wawili walikosa hewa kwenye tanki la maji taka walimokuwa wakirekebisha katika Kituo cha Afya cha Kenyoro, Ekerenyo, kaunti ya Nyamira.

Isaac Maneno Okerio, 40, na Anuri Mauari Nyagaga, 58, walikuwa wakichota maji kutoka kwenye tanki kwa kutumia jenereta walipokosa hewa.

Polisi walipeleka miili hiyo katika chumba cha kuhifadhi maiti cha hospitali ya Nyamira.

Utafsiri: Samuel Maina