Vijana 2 wakamatwa kwa kuteka nyara, kubaka mwanafunzi baada ya 'kumtilia mchele' kwa kileo Kitui

Walimkokota mhasiriwa hadi kwa nyumba ya mmoja wao na kumbaka kwa kupokezana

Muhtasari

•Biron Orwa (25) na Samwel Mulama (22)  wanadaiwa kumpumbaza msichana huyo wa miaka 18  wakiwa katika baa moja mjini Kitui kabla ya kumbeba hadi kwa nyumba ya mmoja wao na kumbaka kwa kupokezana

•Baada ya kupokea ripoti maafisa walivamia nyumba hiyo na kupata msichana yule dhaifu akiwa amelazwa juu ya kitanda huku mshukiwa mmoja amejificha chini ya kitanda akiwa amejawa na woga.tele.

Pingu
Image: Radio Jambo

Polisi upande wa Kitui wanazuilia vijana wawili walioteka nyara na kubaka mwanafunzi wa chuo kikuu.

Biron Orwa (25) na Samwel Mulama (22)  wanadaiwa kumpumbaza msichana huyo wa miaka 18  wakiwa katika baa moja mjini Kitui kabla ya kumbeba hadi kwa nyumba ya mmoja wao na kumbaka kwa kupokezana.

Wapelelezi wa DCI wamebaini kuwa mwanafunzi huyo wa mwaka wa kwanza alikuwa ameandamana na mpenzi wake pamoja na washukiwa hao wawili kupiga maji katika baa ya Monte Christo iliyo Kitui kabla ya tukio hilo kuibuka.

Kulingana na DCI, washukiwa hao wawili ni marafiki wa mpenzi wa mhasiriwa.

Wanne hao walipokuwa kwenye baa, washukiwa waliwaagizia kileo kimoja baada ya kingine hadi mpenzi wa mhasiriwa akalemewa na kujikokota hadi chumbani mwake na kuacha malkia wake mikononi mwa fisi waovu waliokuwa wanammezea mate.

Hapo Orwa na Mulama  wakachukua nafasi hiyo kumbeba mhasiriwa aliyekuwa amepoteza fahamu hadi chumbani cha mmoja wao ambapo walimbaka mmoja baada ya mwingine.

Taarifa ilifikia polisi kuwa vijana wawili walikuwa wameonekana wakiwa wamekokota msichana mdogo aliyekuwa amepoteza fahamu na kumuingiza ndani ya nyumba.

Baada ya kupokea ripoti maafisa walivamia nyumba hiyo na kupata msichana yule dhaifu akiwa amelazwa juu ya kitanda huku mshukiwa mmoja amejificha chini ya kitanda akiwa amejawa na woga.tele.

Mhasiriwa alikimbizwa katika hospitali ya Kitui akiwa katika hali mbaya huku mshukiwa aliyepatikana pale akitiwa pingu.

Mshukiwa wa pili alikamatwa akiwa kwenye baa walimokuwa awali usiku huo ambapo alikuwa ameenda kuchukua viatu na nguo walizokuwa wameanza kumtoa mhasiriwa wao kabla ya kumkokota.

Wawili hao wanatarajiwa kufikishwa mahakamani hivi leo (Ijumaa Julai 30)

Maafisa wa DCI wamehimiza wasichana kutahadhari sana marafiki wanaoandamana nao kwa wakati wote.