Jamaa apiga mkewe hadi kifo, apatikana amezirai kando yake huku amevalia nguo za kike Bungoma

Butwaa kubwa zaidi iliwapiga majirani hao wakati walikuwa katika harakati ya kuomboleza wanandoa hao baada ya Wafula kuamka na kudai dirisha zifunguliwe kuruhusu hewa safi kuingia.

Muhtasari

•Mabonga Wafula kutoka kijiji cha Enamanje maeneo ya Mayanja anadaiwa kumpiga mkewe Elizabeth Mabonga kisha kuzirai kando yake.

•Jirani mmoja ndiye alivutiwa na harufu mbaya iliyokuwa inatoka kwa nyumba ya mshukiwa alipokuwa ameenda kumtembelea Elizabeth. Aliwafahamisha majirani ambao walivunja mlango na kuingia ndani.

POLICE CRIME SCENE
POLICE CRIME SCENE

Polisi upande wa Bungoma wanazuilia mwanaume mmoja anayedaiwa kumpiga mkewe hadi kifo.

Mabonga Wafula kutoka kijiji cha Enamanje maeneo ya Mayanja anadaiwa kumpiga mkewe Elizabeth Mabonga kisha kuzirai kando yake.

Imeripotiwa kuwa marehemu Elizabeth aliwasili pale nyumbani kwao  mnamo Julai 20 baada ya kuhudhuria mazishi ya mamaye wa kambo.

Wakati Elizabeth alipowasili Wafula alikuwa ameenda kupiga maji na aliporejea kwa nyumba akiwa mlevi akaanza kumpiga bila huruma.

Jirani mmoja aliyevutiwa na vurugu iliyokuwa inaendelea pale alijaribu kumshawishi Wafula kusita kumpiga mkewe ila juhudi zake hazikufua dafu. Wafula alimwagiza jirani huyo ajipe shughuli na aache kuwashwa na pilipili asiyoila.

Mwanawe Wafula ambaye alikuwa anashuhudia vita hiyo alikimbia kumuita rafiki wa karibu babake , Barasa Simiyu, ila hakufanikiwa kumpata. Inadaiwa kuwa Wafula angekubali kuskiza ushauri wa Barasa pekee.

Majirani walisema kuwa siku tatu zilizofuata Wafula alionekana akiendelea kupiga maji kama kawaida yake kisha kurudi kwa nyumba kama kwamba hakuna kitu ilikuwa imetendeka.

Jirani mmoja ndiye alivutiwa na harufu mbaya iliyokuwa inatoka kwa nyumba ya mshukiwa alipokuwa ameenda kumtembelea Elizabeth. Aliwafahamisha majirani ambao walivunja mlango na kuingia ndani.

Majirani hao walipigwa na butwaa kuona mwili wa Elizabeth ukiwa unaozea pale ndani huku Wafula  akiwa amelala kando yake akiwa amevalia nguo za marehemu mkewe anayetuhumiwa kuua. Walidhani kuwa wote wawili walikuwa wameaga.

Butwaa kubwa zaidi iliwapiga majirani hao  wakati walikuwa katika harakati ya kuomboleza wanandoa hao baada ya Wafula kuamka na kudai dirisha zifunguliwe kuruhusu hewa safi kuingia.

Maafisa wa polisi walifahamishwa kuhusu tukio hilo na wakafika pale na kumkamata Wafula kisha kupeleka mwili wa Elizabeth mochari.

Mshukiwa anatarajiwa kufanyiwa uchunguzi wa kiakili ili kubaini kama kwamba ako timamu kabla ya  kufikishwa mahakamani.