Kijana anayedaiwa kuua mwanafunzi mpenziwe aliwahi kuua wanafamilia watatu- DCI

Wapelelezi wa DCI wamebaini kuwa Innocent Makhoha, 23, ana rekodi mbaya ya matendo ya kihalifu hapo awali.

Muhtasari

•Makokha ambaye pia ni mwanafunzi katika chuo kikuu cha Mt. Kenya anadaiwa kuua nduguye, mke wake na mtoto wao wa mwaka mmoja.

•Jamaa huyo alikamatwa tena siku ya Jumanne baada ya kuhusishwa na mauaji ya Ambani ambaye alikuwa mpenzi wake.

Makokha na marehemu Christine Ambani anayedaiwa kuua
Makokha na marehemu Christine Ambani anayedaiwa kuua
Image: TWITTER//DCI

Mshukiwa mkuu kwenye mauaji ya Christine Ambani aliyekuwa mwanafunzi wa chuo cha Kisayansi cha Kiriri anadaiwa kuwa gaidi sugu.

Wapelelezi wa DCI wamebaini kuwa Innocent Kalio Makhoha, 23, ana rekodi mbaya ya matendo ya kihalifu hapo awali.

Makokha ambaye pia ni mwanafunzi katika chuo kikuu cha Mt. Kenya anadaiwa kuua nduguye, mke wake na mtoto wao wa mwaka mmoja.

Alikuwa amekamatwa tena mnamo mwezi wa Februari mwaka huu baada ya uchunguzi kubaini aliua nduguye na familia yake kwa kuteketeza nyumba yao wakiwa ndani.

Wapelelezi upande wa Mumias walichunguza kesi hiyo na kuipitisha kwa DPP ili hatua zaidi kuchukuliwa.

"Hata kabla ya wanafamilia hao kuzikwa, Makokha alishambulia familia iliyokuwa inaomboleza kwa kuvuruga mikutano ya kupanga mazishi iliyokuwa inaendelea na kuharibu mali ya familia," ripoti ya DCI ilisema.

Baada ya hayo, Makokha alikamatwa na kushtakiwa kisha kuzuiliwa katika jela ya Kakamega G.K.

Hata hivyo mshukiwa huyo aliachiliwa baada ya kipindi kifupi kufuatia kuondoloewa kwa kesi hiyo katika hali tatanishi.

Makokha alikamatwa tena siku ya Jumanne baada ya kuhusishwa na mauaji ya aliyekuwa mpenzi wake Christine Ambani. 

Inadaiwa kuwa alimdunga Ambani kwenye shingo lake na kuacha mwili wake kwenye chumba cha wageni walichokuwa wamekodishwa maeneo ya Githurai.Mwili wa Ambani ulipatikana mnamo Julai 17.