Equity yafunga tawi la Matuu kufuatia uvamizi ili kupatia nafasi uchunguzi kuendelea

Kiasi cha pesa ambacho hakijathibitishwa kiliibiwa kwenye kwenye benki hiyo

Muhtasari

•Wateja wa benki hiyo walipokea jumbe kuwa tawii hilo litafungwa ili kupatia nafasi uchunguzi kuhusiana na tukio hilo kuendelea.

•Maafisa wa benki walifahamisha wanahabari kuwa ulinzi ulikuwa umewekwa wakati uvamizi huo ulifanyika.

EQUITY BANK MATUU BRANCH
EQUITY BANK MATUU BRANCH
Image: GEORGE OWITI

Habari na George Owiti

Benki ya Equity imetangaza kufungwa kwa tawi la Matuu kufuatia uvamizi uliofanyika Jumanne asubuhi.

Wateja wa benki hiyo walipokea jumbe kuwa tawii hilo litafungwa ili kupatia nafasi uchunguzi kuhusiana na tukio hilo kuendelea.

Benki hiyo ilihimiza wateja wake  kutumia njia mbadala za kupata huduma zake kama vile kadi za benki, Equitel, Ajenti wa Equity, ATM, EazzyApp na zinginezo hadi wakati itafunguliwa tena.

Polisi wameanza uchunguzi kufuatia tukio hilo ambapo kiwango kikubwa cha pesa ambacho hakijabainika bado kiliibiwa.

Maafisa wa benki walifahamisha wanahabari kuwa ulinzi ulikuwa umewekwa wakati uvamizi huo ulifanyika.

Akithibitisha tukio hilo,  kamanda wa polisi upande wa Yatta Mary Njoki alisema kuwa bunduki mbili za maafisa waliokuwa wameshika doria katika benki hiyo ziliibiwa.

Maafisa hao wawili walikimbizwa katika hospitali ya Matuu baada ya kuugua majeraha kufuatia shambulizi la majambazi hao.

Meneja wa tawi hilo Michael Muriithi alipiga ripoti katika kituo cha polisi cha Matuu mida ya saa nne unusu asubuhi.

Aliripoti kuwa genge la majambazi watano lilivamia benki hilo baada ya kushambulia maafisa waliokuwa wameshika doria ,kuwapokonya bunduki zao na kuwaacha na majeraha.

Polisi kutoka kituo cha Matuu walikimbia kwenye eneo la tukio baada ya kufikiwa na taarifa kuhusu uvamizi uliokuwa unaendelea.

Iliripotiwa kuwa baadhi ya wateja waliokuwa wanangoja kuhudumiwa pale waliibiwa pesa walizokuwa nazo.

Mteja mmoja aliibiwa Sh 200,000, mwingine, 51,860, mwingine akaibiwa  Sh11,000, mwingine 3,500 na kunaye aliyeibiwa Sh 4,500.

Kiasi cha pesa ambacho hakijathibitishwa kiliibiwa kwenye kwenye benki hiyo.