Mwanamke 'mwenye pepo' anyonga wanawe wawili kisha kujisalimisha kwa polisi

Alisema kuwa mwanawe wa tatu mwenye umri wa miezi tano alipiga nduru wakati alijaribu kumchukua amuue, hapo ndipo aligundua kuwa alikuwa ametenda mabaya

Muhtasari

•Diana Nasimiyu Kibisu ambaye alionekana kushtuka na kushangaa aliambia maafisa wa polisi kuwa alikuwa ameingiwa na 'pepo mbaya'

•Inadaiwa kuwa Nasimiyu na mumewe Alex Miheso walikuwa na matatizo ya kinyumbani, jambo ambalo bwanake alithibitisha.

•Bosi wa polisi alisema kuwa mwanamke huyo atapelekwa kupimwa akili kabla ya kushtakiwa

POLICE CRIME SCENE
POLICE CRIME SCENE

Mwanamke mmoja aliingia ndani ya kituo cha polisi cha Waithaka, Nairobi usiku wa Jumapili na kutangaza kuwa alikuwa amenyonga wanawe wawili kwa mikono yake.

Diana Nasimiyu Kibisu ambaye alionekana kushtuka na kushangaa aliambia maafisa wa polisi kuwa alikuwa ameingiwa na 'pepo mbaya'

DCIO wa Dagoretti Francis Wahome alimdondoa  Nasimiyu akisema kuwa alikuwa karibu kumuua mwanawe wa tatu.

"Alisema kuwa mwanawe wa tatu mwenye umri wa miezi tano alipiga nduru wakati alijaribu kumchukua amuue, hapo ndipo alifahamu kuwa alikuwa ametenda mabaya"  Wahome alisema.

Alisema kuwa mwanamke huyo alijuta matendo yake na hangeweza kuelezea mbona akayatenda.

Mwanamke huyo alikamatwa baada ya kuwaongoza polisi hadi kwa nyumba yake alipotendea unyama huo kwa wanawe wa miaka 4 na 2.

Polisi walisema kuwa walipata miili wa Sydney Miheso, 4, na Miracle Miheso, 2, ikiwa imelazwa juu ya sofa iliyokuwa  ndani ya sebule.

Bosi wa polisi alisema kuwa mwanamke huyo atapelekwa kupimwa akili kabla ya kushtakiwa.

Inadaiwa kuwa Nasimiyu na mumewe Alex Miheso walikuwa na matatizo ya kinyumbani, jambo ambalo bwanake alithibitisha.

Inasemekana kuwa mamaye Miheso alikuwa amesafiri kutoka Lugari kwa juhudi za kuwapatanisha wawili hao ila hazikufua dafu.

Miheso alisema kuwa wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ila hakuwa anatarajia mkewe kuangamiza watoto wao.

"Alinipiga simu na kuniomba nifike nyumbani kwani alikuwa ameua watoto. Amekuwa akinitumia jumbe akitishia kuwaua" Miheso alisema.

(Utafsiri; Samuel Maina)