Polisi wachanga karo ya mwanafunzi aliyejaribu kujitoa uhai kwa kutojiunga na sekondari, Muranga

Inadaiwa kuwa Muthoni alikuwa amejaribu kujitoa uhai baada ya kuona kuwa wenzake walikuwa wamejiunga na shule za upili ilhali yeye alisalia tu nyumbani.

Muhtasari

•Kwa kipindi cha wiki mbili zilizopita wanafunzi wa kidato cha kwanza  wamekuwa wakijiunga na shule za upili walizoitwa ila Linet Muthoni hakuwa amejiunga na shule yoyote kwa kukosa karo.

•Inadaiwa kuwa Muthoni alikuwa amejaribu kujitoa uhai baada ya kuona kuwa wenzake walikuwa wamejiunga na shule za upili ilhali yeye alisalia tu nyumbani. Kesi hiyo iliripotiwa katika kituo cha polisi cha Maragua na hapo ndipo OCS Cleophas Juma alianza juhudi za kusaidia familia. 

Linet Muthoni, wazazi wake na wasamaria wema katika shule ya upili ya Kiangunyi Girls, Kangema
Linet Muthoni, wazazi wake na wasamaria wema katika shule ya upili ya Kiangunyi Girls, Kangema
Image: ALICE WAITHERA

Familia moja upande wa Muranga ni yenye furaha baada ya maafisa wa polisi kutoka kituo cha Maragua kuwasaidia kupeleka binti wao katika shule ya upili.

Kwa kipindi cha wiki mbili zilizopita wanafunzi wa kidato cha kwanza  wamekuwa wakijiunga na shule za upili walizoitwa ila Linet Muthoni hakuwa amejiunga na shule yoyote kwa kukosa karo.

Wazazi wake ambao hutegemea kupata vibarua hapa na pale ili kukimu mahitaji ya familia walikuwa wameshindwa kupata fedha za kumpeleka mtoto wao katika shule ya Kiangunyi Girls Secondary ambako alikuwa ameitwa.

Inadaiwa kuwa Muthoni alikuwa amejaribu kujitoa uhai baada ya kuona kuwa wenzake walikuwa wamejiunga na shule za upili ilhali yeye alisalia tu nyumbani.

Kesi hiyo iliripotiwa katika kituo cha polisi cha Maragua na hapo ndipo OCS Cleophas Juma alianza juhudi za kusaidia familia. 

Juma aliomba usaidizi wa baadhi ya maafisa na wadau wengine hadi wakapata mchango tosha wa kumsaidia Muthoni kujiunga na sekondari.

Baada ya kuthibitisha kuwa alikuwa amepata kiasi tosha cha pesa, OCS Juma alimpigia mama ya Muthoni simu na kumwambia afike katika kituo cha polisi. Mwendesha bodaboda alitumwa kumchukua pamoja na bintiye ili waweze kufika kituoni.

Walipofika kituoni walifahamishwa kuwa fedha walizokuwa wanahitaji zilikuwa zimepatikana na hapo wakajawa na bashasha.

Mama ya Muthoni, Lucy Wangechi alisema kuwa alikuwa na wasiwasi baada ya kuambiwa kuwa alikuwa anahitajika katika kituo cha polisi kwani alifahamu kuwa kwa mara nyingi watu huitwa kituoni kwa kuhusishwa na uhalifu.

Baada ya kupashwa habari hizo njema, Muthoni na mamaye walipelekwa mjini Thika ambapo walinunuliwa sare za shule na vitu zingine za matumizi.

Baada ya kukamilisha shughuli ya ununuzi maafisa kadhaa walimzidikisha Muthoni hadi shuleni ambapo alipokewa vyema.