Mchuuzi aliyepigwa na maafisa wa kaunti anaendelea kupona baada ya kufanyiwa upasuaji

Maina alipokea huduma hizo zote bila malipo..

Muhtasari

•Maina alipoteza meno matano na taya lake kuvunjika mikononi mwa maafisa wa ukaguzi jijini Nairobi waliomshambulia baada yake kukosa kuwapatia hongo ya shilingi mia moja.

•Mapema wiki iliyopita maafisa watatu wa kaunti ya Nairobi walikuwa wamekubali kumlipa Maina shilingi 427,200 kama fidia baada ya kumshambulia na kumng'oa meno matano.

Picha ya Maina ya awali na ya sasa
Picha ya Maina ya awali na ya sasa
Image: ORTHODONTICS KENYA

Hatimaye Anthony Maina, mchuuzi anayedaiwa kung'olewa meno na maafisa wa kaunti ya Nairobi anaweza kutabasamu kwa sasa baada ya kupokea matibabu.

Maina alipoteza meno tano na taya lake kuvunjika mikononi mwa maafisa wa ukaguzi jijini Nairobi waliomshambulia baada yake kukosa kuwapatia hongo ya shilingi mia moja.

Mnamo Jumapili, Daktari Kennedy Carson Opiyo kutoka Orthodontics Kenya alisema kuwa Maina alikuwa anaendela kupona baada ya meno yake kurekebishwa.

"Taya lake lilikuwa limeharibika, kuna meno yake kadhaa yaliyokuwa karibu kuanguka na alikuwa amejiuma vibaya" Opiyo alisema.

Opiyo alifichua kuwa taya la chini la Maina lilikuwa limeathirika vibaya kwani lilikuwa limevunjika mara mbili.

Maina anaendelea kupona na hali yake itaangaliwa tena baada ya wiki mbili. Alipokea huduma hizo  zote bila malipo..

"Baada ya tukio hilo kuangaziwa sana, wateja wetu walituomba kumsaidia Maina kwa hivyo tukaamua kumsaidia bila malipo" Daktari Opiyo alisema.

Mnamo Julai 2 mchuuzi kwa jina Anthony Maina ambaye huuza soksi maeneo ya CBD  alishambuliwa na askaris wa kaunti ya Nairobi na kupoteza meno kadhaa.

Alisema kuwa maafisa hao walikuwa wanadai awapatie shilingi 100 ila alikuwa na shilingi 20 peke yake. Kufuatia hayo maafisa hao wakampiga vibaya.

Mapema wiki iliyopita maafisa watatu wa kaunti ya Nairobi walikuwa wamekubali kumlipa Maina shilingi 427,200 kama fidia baada ya kumshambulia na kumng'oa meno matano.

Katika juhudi za kuepuka mashtaka na kufutwa kazi Humprey Muswangi, Hassan Chege na Dennis Macharia walikubali kusuluhisha kesi hiyo nje ya mahakama mnamo Jumanne wiki iliyopita.