Butwaa baada ya wavuvi 'kuvua' bomu 6 katika ziwa Victoria

Kwa hofu kuwa bomu zile zingelipuka wawili kati yao waliamua kujitosa ndani ya ziwa na kuacha wenzao watatu wasijue la kufanya

Muhtasari

•Kulingana na DCI, wavuvi hao walitupa wavu ndani ya maji wakitarajia kunasa samaki na hapo ndipo wavu wao ulinasa kitu kilichokuwa na uzito usio wa kawaida.

•Kwa ushirikiano watano hao wakavuta wavu ule wakisubiri kwa hamu kumchukua samaki mkubwa waliyenasa ila salaalaa! butwaa kubwa iliwapiga kuona kuwa wavu wao ulikuwa umenasa kijisanduku cha chuma.

Image: TWITTER//DCI

Hali ya wasiwasi ilitanda maeneo ya  Mbita kaunti ya Homabay baada ya wavuvi watano waliokuwa katika harakati ya kazi yao ziwani Victoria kupata bomu 6 kutoka ndani ya ziwa hilo.

Kulingana na DCI, wavuvi hao walitupa wavu ndani ya maji wakitarajia kunasa samaki na hapo ndipo wavu wao ulinasa kitu kilichokuwa na uzito usio wa kawaida.

Mwanzoni walidhani kuwa walikuwa walikuwa na bahati ya mtende kumkamata samaki mkubwa na kwa furaha wakashirikiana kuvuta wavu kutoka ndani ya maji ili wachukue vuno lao.

Kwa ushirikiano watano hao wakavuta wavu ule wakisubiri kwa hamu kumchukua samaki mkubwa waliyenasa ila salaalaa! butwaa kubwa iliwapiga kuona kuwa wavu wao ulikuwa umenasa kijisanduku cha chuma.

Kwa hamu wakafungua sanduku lile ili kujua kilichokuwa mle ndani na hawakuamini macho zao kuona bomu sita zikiwa zimepangwa pale.

Kwa hofu kuwa bomu zile zingelipuka wawili kati yao waliamua kujitosa ndani ya ziwa na kuacha wenzao watatu wasijue la kufanya. Baada ya majadiliano mafupi wavuvi watatu waliobaki waliafikiana kuenda kumfahamisha meneja wa ufuko eneo lile Bw Isaiah Ouko ambaye alipiga ripoti kwa wapelelezi wa DCI.

Wapelelezi wa DCI walifahamisha wataalamu wa kuharibu bomu kutoka Kisumu ambao walichukua shehena ile kuifanyia uchunguzi kisha kuiharibu.