CHANZO CHA MZOZO HAKIJABAINIKA

Hofu Kiambu baada ya mwanabiashara kum'miminia mkewe risasi kisha kujitoa uhai

Mukundi ambaye ni mmiliki wa bunduki kihalali alimpiga mkewe risasi tatu kabla ya kujitoa uhai kwa kujipiga risasi kichwani

Muhtasari

•Polisi walipata miili ya Jonathan Mukundi Gachunga (42) na mkewe Philomena Njeri (30) ilipatikana ndani ya chumba chao cha kulala baada ya rafiki wao wa karibu kuwafahamisha kuwa Gachunga hakuwa anashika simu zake, jambo ambalo si la kawaida.

•Polisi wameanza  uchunguzi kuhusiana na tukio hilo ingawa chanzo cha mzozo uliosababisha maafa hayo bado hakijabainishwa.

Jonathan Mukundi na bibiye Philomena Njeri
Jonathan Mukundi na bibiye Philomena Njeri
Image: HISANI

Hali ya hofu ilitanda katika maeneo ya Kirigiti kaunti ya Kiambu baada ya wanandoa wawili kupatikana wameaga dunia nyumbani kwao Jumanne jioni.

Polisi walipata miili ya mwanabiashara Jonathan Mukundi Gachunga (42) na mkewe Philomena Njeri (30) ilipatikana ndani ya chumba chao cha kulala baada ya rafiki wao wa karibu kuwafahamisha kuwa Gachunga hakuwa anashika simu zake, jambo ambalo si la kawaida.

Kulingana na ripoti ya polisi, Mukundi ambaye ni mmiliki wa bunduki kihalali alimpiga mkewe risasi tatu  kabla ya kujitoa uhai kwa kujipiga risasi kichwani.

Bastola ya mwanabiashara huyo ilipatikana katika eneo la tukio.

Polisi wameanza  uchunguzi kuhusiana na tukio hilo ingawa chanzo cha mzozo uliosababisha maafa hayo bado hakijabainishwa.

Miili ya wanandoa hao ilipelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha hospitali kuu ya Kenyatta huku upasuaji wa miili ukisubiriwa.

Aliyekuwa gavana wa Nairobi Mike Sonko ni mmoja wa ambao wamelaani kitendo hicho akisema kuwa suala la  mauaji dhidi ya wanawake linafaa kuangaziwa.

Sonko ameshauri wanaume kujiepusha na hasira kwani yaweza kusababisha madhara makubwa.

"Hii mambo ya wanaume kuuwa bibi zao sasa imekithiri. Mauaji dhidi ya wanawake yamekuwa mengi sana nchini Kenya na nafikiri kuwa tunafaa kutafuta njia ya kutafuta suluhu ya kesi hizi kwa kina.. Hii maisha ni fupi sana tupunguzeni hasira ama tuwache hasira kwa baa" Sonko alisema.