Wezi wampatia mbwa mlinzi sumu katika jaribio la wizi lililoaacha mmoja wao akiwa maiti, Kakamega

Baada ya kugundua kuwa mipango yao ilikuwa imeharibiwa washukiwa hao waliamua kutimua mbio kuokoa maisha yao ila wanakijiji wenye ghadhabu wakamkamata mmoja wao na kumpiga vibaya.

Muhtasari

•Inaaminika kuwa kabla ya jaribio la kuvamia nyumba ya mwanamke aliyetambulishwa kama Mirriam Miramboga, washukiwa hao walikuwa wamewasili mapema na kumpa sumu mbwa aliyekuwa analinda nyumba hiy

•Ole wao mwenye nyumba hakuwa amelala na alipogundua vivuli vya watu vikisonga nje ya nyumba yake. Hapo Miramboga akapiga mayowe makali yaliyoamsha majirani na wanakijiji wengine waliojitokeza kwa wingi kusaidia.

crime scene 1
crime scene 1

Juhudi za washukiwa wawili wa wizi ziliangulia patupu baada ya mwenye nyumba waliyolenga kuvamia katika kijiji kimoja maeneo ya Lugari, Kakamega kuwaona na kupiga nduru iliyoaamsha wanakijiji wengine.

Inaaminika kuwa kabla ya jaribio la kuvamia nyumba ya mwanamke aliyetambulishwa kama Mirriam Miramboga, washukiwa hao walikuwa wamewasili mapema na kumpa sumu mbwa aliyekuwa analinda nyumba hiyo.

Baada ya mbwa yule kuangamizwa na sumu washukiwa hao walijitokeza kutoka mafichoni mida ya saa saba usiku na kuingia kwake Miramboga tayari kutekeleza wizi.

Ole wao mwenye nyumba hakuwa amelala na alipogundua vivuli vya watu vikisonga nje ya nyumba yake. Hapo Miramboga akapiga mayowe makali yaliyoamsha majirani na wanakijiji wengine waliojitokeza kwa wingi kusaidia.

Baada ya kugundua kuwa mipango yao ilikuwa imeharibiwa washukiwa hao waliamua kutimua mbio kuokoa maisha yao ila wanakijiji wenye ghadhabu wakamkamata mmoja wao na kumpiga vibaya.

Polisi kutoka  kituo cha Lumakanda walifika kwenye eneo hilo na kujaribu kumuokoa mshukiwa aliyekuwa ameumizwa vibaya ila alikata roho hata kabla ya kufika hospitalini.

Mwili wa marehemu ulipelekwa katika mochari ya Webuye huku utambulisho ukisubiriwa.