5 wafariki, 1 hospitalini Nakuru baada ya kunywa chang'aa inayotuhumiwa kuwa na sumu

Miili ya wahasiriwa wanne ilipatikana katika maeneo tofauti ilhali mmoja wao alifariki alipokuwa anapokea matibabu katika hospitali ya Bahati.

Muhtasari

•Sita hao wanadaiwa kunywa tembo iliyokuwa na sumu jioni ya Jumatatu katika baa moja maeneo ya Kabatini, Nakuru Kaskazini.

•Kamanda wa polisi maeneo ya Nakuru Beatrice Kiraguri alisema kuwa haijabainika wazi kileo walichokunywa kwani hakuna mtu aliyetaka kutoa habari  yeyote kuhusiana na tukio hilo.

crime scene 1
crime scene 1

Watu watano walifariki na mmoja kulazwa hospitalini katika kaunti ya Nakuru baada ya kunywa changaa inayotuhumiwa kuwa ilikuwa imetiwa sumu.

Sita hao wanadaiwa kunywa tembo iliyokuwa na sumu jioni ya Jumatatu katika baa moja maeneo ya Kabatini, Nakuru Kaskazini.

Kulingana na wakazi wa maeneo hayo, mhasiriwa aliyenusurika kifo alianza kulalamikia  kuumwa na tumbo kisha kuzirai na hapo ndipo akakimbizwa hospitalini akiwa hali mahututi.

Miili ya wahasiriwa wanne ilipatikana katika maeneo tofauti ilhali mmoja wao alifariki alipokuwa anapokea matibabu katika hospitali ya Bahati.

Kamanda wa polisi maeneo ya Nakuru Beatrice Kiraguri alisema kuwa haijabainika wazi kileo walichokunywa kwani hakuna mtu aliyetaka kutoa habari  yeyote kuhusiana na tukio hilo.

"Hata aliyenusurika hawezi kusema walichokunywa.. ni kiongozi wa maeneo hayo ambaye ametufahamisha kuwa inatuhumiwa walikunywa chang'aa iliyokuwa na sumu" Bi Kiraguri alisema.

Bi Kiraguri alisema kuwa sampuli zilikuwa zimechukuliwa kutoka kwa wahasiriwa walioaga na aliyenusurika ili kuthibitisha wazi kilichosababisha madhara hayo.

"Kuna madai kuwa chang'aa ile ilikuwa imetiwa sumu na mshindani mmoja wa muuzaji  ambaye amekuwa akidai kuwa mali yake imekuwa ikiibiwa. Hata hivyo, tunachukulia hayo kama uvumi tu hadi tupate mashahidi watakaothibitisha" Kiraguri alisema.

Mhasiriwa aliyenusurika anaendelea kupokea matibabu katika hospitali ya bahati ilhali miili ya watano waliofariki imehifadhiwa katika mochari ya Bahati.