Baadhi ya sababu kwa nini wanaume huhofia kuoa wanawake wenye umri mkubwa kuwashinda

Wanaume ambao huoa wake wenye umri mkubwa kwa mara nyingi hukosolewa sana na hujipata wakipokea upinzani mkubwa kutoka kwa jamii kufuatia maamuzi yao.

Muhtasari

•Mwanaume aweza kupata kipenzi cha moyo wake kisha akakosa kumuoa baada ya kugundua kuwa amempiku kwa umri kwa hofu ya kusemwa na jamii.

•Kuna hofu miongoni mwa jamii kuwa huenda mwanamke mwenye umri mkubwa kuliko mumewe akakosa kumpa heshima kwa kuwa ameishi miaka mingi na kuona mengi kumliko.

Pete
Pete
Image: SERENDIPITY DIAMONDS

Ni dhahiri kuwa asilimia kubwa ya wanaume wanapendelea kuchumbia na kuoa wanawake ambao wana umri mdogo kuwashinda.

Hili ni jambo la kawaida kote ulimwenguni na ukiangazia ndoa nyingi utagundua kuwa aghalabu mwanaume huwa amempiku mkewe na angalau mwaka mmoja kwenda juu.

Ingawa haijanakiliwa kwa Bibilia ama kutajwa kama mojawapo ya mila na desturi za jamii, sio wanaume wengi utakaopata wakikubali kufunga ndoa na wanawake wenye umri mkubwa  kuwashinda.

Wanaume ambao huoa wake wenye umri mkubwa  kwa mara nyingi hukosolewa sana na hujipata wakipokea upinzani mkubwa kutoka kwa jamii kufuatia maamuzi yao.

Kunazo sababu kwa nini wanaume huogopa kujiingiza kwa ndoa ambapo wao ndio wadogo kuliko wake zao;-

1. Kuogopa kusemwa na jamii

Mwanaume aweza kupata kipenzi cha moyo wake kisha akakosa kumuoa baada ya kugundua kuwa amempiku kwa umri kwa hofu ya kusemwa na jamii.

Jambo hili limewatendekea wengi ambao hushinikizwa na itikadi zilizoko miongoni mwa jamii kuhusiana na kuoa mke aliye na umri mkubwa

Wengine huogopa kuchekwa na kutusiwa kwani hilo ni jambo la kawaida haswa hapa nchini Kenya. 

Kunao baadhi ya wanaume mashuhuri ambao wamejipata wakikosolewa sana na Wakenya baada yao kufunga ndoa na wanawake wazee kuwaliko.

Wanajamii wengi hawachukulii jambo hilo kuwa la kawaida.

2. Heshima

Kitu moja ambacho hufanikisha kufaulu kwa ndoa ni heshima kati ya wapendanao.  Kunazo ndoa nyingi ambazo zimevunjika kufuatia ukosefu wa heshima.

Kuna hofu miongoni mwa jamii kuwa huenda mwanamke mwenye umri mkubwa kuliko mumewe akakosa kumpa heshima kwa kuwa ameishi miaka mingi na kuona mengi kumliko.

Inaaminika kuwa akili ya mwanamke hukomaa haraka kushinda ya mwanaume na kuna msemo unaotumika sanaunaosema kuwa 'Mwanaume na mwanamke wenye umri sawa hawako sawa kimawazo"'

3. Itikadi kuwa wanawake huzeeka haraka kushinda wanaume

Jinsi wanaume huzeeka ni tofauti na wanawake wanavyozeeka. Wanawake hupata mabadiliko makubwa ya homoni zaidi ya wanaume na jambo hilo laweza  kufanya waonekane wazee kushinda wenzao wa kiume wa rika moja.

Hili ni jambo lingine ambalo hufanya baadhi ya wanaume kuhofia kujitosa kwenye ndoa na wanawake wenye umri mkubwa kuwashinda.

Wasiwasi kuwa wake zao huenda wakazeeka haraka huwashinikiza kutafuta wanawake wenye umri mdogo kuwashinda.

Inaamika kuwa wanawake wanapofikisha umri wa miaka 55 wengi wao hupoteza uwezo wa kubeba mimba. Huenda mwanaume akaogopa  kuoa mwanamke anayekaribia kufikisha umri huo kwa hofu kuwa hataweza kupata mtoto.

4. Tamaduni

Kunazo baadhi ya jamii barani Afrika ambazo huamini kuwa kitendo cha kuoa mke mzee kukushinda ni mwiko.

Kunazo jamii ambazo huruhusu wanaume wenye umri mkubwa kulipa mahari ya msichana mdogo na kusubiri hadi abalehe ili amuoe rasmi.

Jamii kama hizo hushikilia tamaduni kuwa mwanaume anafaa kuoa mwanamke mdogo kwani vile ndoa itaweza kustawi na kuwa na heshima.