Mwanamke mjamzito apoteza uwezo wa kuona baada ya kunywa chang'aa yenye sumu Nakuru

Wengine 3 wanaendelea kupokea matibabu katika hospitali ya Bahati huku ikiripotiwa kuwa mmoja wao bado hajarejesha fahamu

Muhtasari

•Mwanamke mmoja mjamzito ambaye ni miongoni mwa waliokunywa pombe yenye sumu iliyosababisha vifo vya watu watano anaendelea kupokea matibabu maalum katika hospitali ya rufaa ya Nakuru baada yake kupofuka.

•Gavana Lee Kinyajui amesema kuwa vita za hivi karibuni dhidi ya vileo haramu katika maeneo hayo hazikuwa zimefua dafu kwani kunao baadhi ya maafisa wa kulinda usalama ambao wamejitosa kwenye biashara ile.

Image: MAKTABA

Mwanamke mmoja mjamzito ambaye ni miongoni mwa waliokunywa pombe yenye sumu iliyosababisha vifo vya watu watano anaendelea kupokea matibabu maalum katika hospitali ya rufaa ya Nakuru baada yake kupofuka.

Katika ziara yake ya kufariji familia zilizofiwa, gavana Lee Kinyajui alisema kuwa mwanamke huyo alihamishwa kupelekwa hopitali ya Nakuru baada ya madaktari kugundua kuwa alikuwa amepoteza uwezo wa kuona.

Watu wengine watatu walionusurika kifo baada ya kubugia kileo hicho hatari wanaendelea kupokea matibabu katika hospitali ya Bahati huku ikiripotiwa kuwa mmoja wao bado hajarejesha fahamu.

Gavana Kinyajui alisema kuwa ni jambo la kuhuzunisha kuona kwamba kunao baadhi ya vijana katika kijiji ambacho mkasa ulitokea  ambao wanaendelea kulewa chang'aa hata baada ya vifo kuripotiwa.

Alisema kuwa vita za hivi karibuni dhidi ya vileo haramu katika maeneo hayo hazikuwa zimefua dafu kwani kunao baadhi ya maafisa wa kulinda usalama ambao wamejitosa kwenye biashara ile.

"Tumeendelea kulaani hadharani uuzaji na unywaji wa pombe haramu ambayo inawaacha vijana wetu bila uwezo wa kuzalisha na wengine kuaga" Kinyajui alisema.

Gavana huyo aliwasihi wakazi kuwaripoti wote ambao wanajihusha na biashara ya kuuza pombe isiyokubalika.

Wakazi walisema kuwa vifo kutokana na unywaji wa pombe haramu ni jambo la kawaida katika maeneo hayo.