Polisi 5 wa Ruiru waliomuibia jamaa 1,030 wakamatwa kwa kosa la wizi wa mabavu

Mmoja wa maafisa hao alichukua simu ya jamaa huyo, akamwagiza amfichulie pini yake na kutuma shilingi 1,030 kwa namba nyingine.

Muhtasari

•Makonstabo hao wanadaiwa kukamata jamaa mmoja mnamo Agosti 12 maeneo ya Ruiru kwa kukiuka sheria za kafyu kisha kumuibia

• Mmoja wa maafisa hao alichukua simu ya jamaa huyo, akamwagiza amfichulie pini yake na kutuma shilingi 1,030 kwa namba nyingine.

Kamanda wa polisi Kiambu, Ali Nuno
Kamanda wa polisi Kiambu, Ali Nuno
Image: HISANI

Polisi watano walikamatwa usiku wa Jumanne kwa tuhuma za wizi wa mabavu walipokuwa katika harakati za kutekeleza mikakati iliyowekwa kudhibiti janga la Corona.

Makonstabo hao wanadaiwa kukamata jamaa mmoja mnamo Agosti 12 maeneo ya Ruiru kwa kukiuka sheria za kafyu kisha kumuibia.

 Mmoja wa maafisa hao alichukua simu ya jamaa huyo, akamwagiza amfichulie pini yake na kutuma shilingi 1,030 kwa namba nyingine.

Kulingana na mlalamishi, polisi huyo alituma pesa kwa namba nyingine kisha kufuta ujumbe wa Mpesa.

"Alifanya hivyo ili nisitume ujumbe wa kurejeshewa pesa zangu kwa 456" mlalamishi alisema.

Kamanda wa polisi maeneo ya Kiambu Ali Nuno amesema kuwa uchunguzi uling'oa nanga baada yake kuona malalamiko kuhusu tukio hilo kwenye mitandao ya kijamii.

"Tulithibisha kuwa kulikuwa na ishara za wizi. Walimfunga pingu jamaa huyu na wakiwa wamejihami kwa bunduki wakachukua simu yake na kutuma pesa kwa namba zao" Ali alisema.

Ali alisema kuwa kesi hiyo ilikuwa imepelekwa mahakamani ambako walipata kibali cha kuchunguza namba za simu za maafisa hao kama hatua moja ya uchunguzi.

Watano hao watashtakiwa kwa kosa la wizi wa mabavu .

Mhudumu wa duka la Mpesa ambalo lilitumika kutekeleza shughuli ile pamoja na mwajiri wake  walikamatwa pia na watasaidia polisi katika uchunguzi.