Bado sijafutilia mbali kufanya kazi na Ruto- Gavana Waiguru

Amesema kuwa bado ni mapema sana kuzungumzia suala la iwapo anaweza kujiunga na UDA.

Muhtasari

•Gavana huyo alifunguka kuhusu mipango yake ya kisiasa ya  2022 akisema kwamba hata kama hawezi kutangaza wazi iwapo atajiunga na UDA, watu wa Kirinyaga ndio watafanya maamuzi ya mwisho.

•Siku ya Jumamosi Waiguru alidai kuwa tume ya EACC ilikuwa inamlenga baada ya matamshi yake kuwa eneo la Mt Kenya linafaa kurejelea majadiliano baada ya kuanguka kwa BBI.

Gavana wa Kirinyaga Anne Mumbi
Gavana wa Kirinyaga Anne Mumbi
Image: MAKTABA

Gavana wa Kirinyaga Anne Waiguru amefichua kwamba hawezi kufutilia mbali kufanya kazi na naibu rais William Ruto katika uchaguzi mkuu wa 2022.

Hata hivyo Waiguru amesema kuwa bado ni mapema sana kuzungumzia suala la iwapo anaweza kujiunga na UDA.

Gavana huyo alifunguka kuhusu mipango yake ya kisiasa ya  2022 akisema kwamba hata kama hawezi kutangaza wazi iwapo atajiunga na UDA, watu wa Kirinyaga ndio watafanya maamuzi ya mwisho.

Hivi karibuni gavana Waiguru amekuwa akionyesha dalili za kubadili mkondo wake wa kisiasa haswa baada ya mahakama kutupilia mbali mchakato wa BBI.

"Siwezi kusema iwapo naweza kujiunga na UDA au la. Unajua hizi ni siasa, lakini sio jambo rahisi kutendeka, ni mapema sana. Wacha tuone vile hali ilivyo uwanjani" Waiguru alisema katika stesheni moja ya Radio nchini siku ya Jumatatu.

Siku ya Jumamosi Waiguru alidai kuwa tume ya EACC ilikuwa inamlenga baada ya matamshi yake kuwa eneo la Mt Kenya linafaa kurejelea majadiliano baada ya kuanguka kwa BBI.

Waiguru alidai kuwa aliitwa na EACC  punde baada yake kusema kuwa kuna haja ya eneo la Mt Kenya kujichunguza.