Mwanamume ahukumiwa kifungo cha miaka 30 jela kwa kumuua kasisi wa Machakos

Muhtasari
  •  Mwanamume ahukumiwa kifungo cha miaka 30 jela kwa kumuua kasisi wa Machakos
Image: Benjamin Njuguna

Mahakama ya Embu imemhukumu Michael Mutunga kifungo cha miaka 30 jela baada ya kupatikana na hatia ya kumuua kasisi wa Kanisa Katoliki Michael Maingi mwaka wa 2019.

Jaji Lucy Njuguna Alhamisi, alisema hakuna uhalali wa hatua ya Mutunga.

Mutunga kupitia kwa Wakili wake Kirimi Gwantai alikuwa ametumia kigezo cha kupunguza hali iliyoashiria kuwa hatua yake ilikuwa ya huzuni na hasira baada ya kulawitiwa na kasisi huyo.

Jaji Lucy alisema Mutunga alipaswa kutumia njia za kisheria zilizopo kutafuta haki badala ya kuchukua suala hilo mikononi mwake.

Alisema tabia ya mshtakiwa huyo baada ya kutenda kosa hilo inasaliti kuwa hana hatia kwa njia zote baada ya kutoa sh 400,000 kwenye M-pesa ya marehemu, kukamata gari lake na kuligeuza kuwa lake.

"Ninaona mazingira ambayo kosa hili lilifanyika yalihitaji hukumu kali. Ninamhukumu mshtakiwa wa kwanza miaka 30 jela," hakimu alisoma.

"Tayari nimezingatia muda ambao amekuwa chini ya ulinzi."

Kwa upande wake, kasisi Francis Maundu wa Dayosisi ya Machakos alisema amefurahishwa na hukumu hiyo.

Mutunga alikuwa pamoja na washtakiwa wengine wawili Kavivya Mwangangi na Solomon Mutava ambao kesi yao itatajwa tarehe 17 Novemba.

Mutunga alipatikana na hatia ya kumuua Maingi mnamo Oktoba 8, 2019 na kumzika kwenye kaburi la kina kifupi kando ya mto Mashamba wa msimu huko Makima huko Mbeere Kusini huko Embu.