Familia ya mtoto Yasini Moyo ingali kupata haki, miaka 2 baada ya kifo chake

Muhtasari

• Kesi ya mauaji ya kijana Yasin Moyo imegoma kuendelea baada ya wakili wa utetezi kukosa kufika mahakamani.

• Yasin Moyo, 13, ambaye aliuawa kwa kupigwa risasi na polisi mapema mwaka wa 2020 wakati wa utekelezaji wa amri ya kutotoka nje usiku, alifariki baada ya polisi kwa jina Duncan Ndiema kumfyatulia risasi akiwa katika roshani ya nyumba yao katika mtaa wa mabanda wa Mathare, jijini Nairobi.

Yasini Moyo graffiti
Missing Voices KE (Facebook) Yasini Moyo graffiti

Kesi ya mauaji ya Yasin Moyo imekosa kuendelea baada ya wakili wa mshtakiwa kukosa kufika mahakamani.

Yasin Moyo, 13, ambaye aliuawa kwa kupigwa risasi na polisi mapema mwaka wa 2020 wakati wa utekelezaji wa amri ya kutotoka nje usiku, alifariki baada ya polisi kwa jina Duncan Ndiema kumfyatulia risasi akiwa katika roshani ya nyumba yao katika mtaa wa Mathare, jijini Nairobi.

Kulingana na taarifa iliyochapishwa na shirika la Missing Voices Kenya,  kesi hiyo ilitarajiwa kuendelea tena Januari 24 mwaka wa 2022 baada ya polisi huyo awali kukana mashitaka ya mauaji ya kijana huyo, wakili Dansten Omari ambaye anawakilisha upande wa utetezi alikosa kufika mahakamani.

Mahakama iliambiwa kwamba wakili Omari hangeweza kufika mahakamani kwa kesi hiyo kutokana na kwamba alikuwa tayari jijini Mombasa kwa kesi nyingine ya mauaji inayomhusu mbunge Aisha Jumwa.

Kesi hiyo ya mauaji ya Yasin Moyo ilikuwa tayari imepangiwa kuendelea na mashahidi wanne akiwemo mwanafunzi wa shule ya upili walikuwa wametayarishwa kutoa ushahidi.

Mahakama
Mahakama

Akiwakilisha upande wa wahasiriwa, wakili Janice Muchemi kutoka shirika la International Justice Mission alisema kwamba ni jambo la kusononesha kwamba kesi hiyo bado imekwama na haki kupatikana kwa Yasini, miaka miwili tangu kukatizwa kwa Maisha yake kwa mtutu wa bunduki ya polisi mhuni.

“Mheshimiwa, kesi hii iliratibiwa kuanza januari mwaka 2022, siku ambazo zilichaguliwa kwa ridhaa ya pande zote husika. Naiomba mahakama hii izingatie kuwa tukio hili lilitokea mwaka wa 2020 na mpaka sasa tayari tushaingia 2022 lakini bado hakuna kitu chochote kinachoendelea.” Aliteta wakili Muchemi.

Mahakama iliamuru kutengwa kwa tarehe mpya ya kesi hiyo ili familia ya marehemu Yasini Moyo wapate haki.

Mtuhumiwa huyo Duncan Ndiema ambaye baada ya kukana mashataka ya mauaji ya mtoto huyo na ambaye kwa sasa yuko nje kwa dhamana, alipandishwa kizimbani baada ya uchunguzi Madhubuti wa mamlaka ya uangalizi huru wa polisi.

Hii ni kesi moja kati yqa kesi zingijne nyingi tu nchini Kenya zinazowahusu polisis na utumiaji mbaya wa bunduki zao, hasa katika kipindi cha utekelezaji wa amri ya kutotoka nje usiku kama njiqa moja ya kudhibiti kuzambaa kwa virusi vya Corona.

Itakumbukwa pia kuna kesi nyingine ambayo iko mahakamani inayowahusisha polisi sita wanaoshukiwa kutekeleza mauaji ya vijana wawili kutoka eneo la Kianjokoma, kaunti yqa Embu.