Nilipatikana na maambukizi ya covid-19 mwezi jana-Francis Atwoli

Muhtasari
  • Aliwashauri Wakenya kuendelea kupata chanjo kwani chanjo imesaidia sana katika vita dhidi ya covid-19
FRancis Atwoli
Image: Mercy Mumo

Katibu Mkuu wa COTU Francis Atwoli amesema kwamba alipatikana na maambukizi ya Covid-19 lakini hayakuwa na athari kubwa kwake.

Akizungumza katika Chuo cha Kazi cha Tom Mboya Jumanne, Atwoli alisema kuwa ugonjwa haukuwa na athari kubwa kwa sababu alikuwa amepokea chanjo dhidi ya maambukizi hayo.

"Niliambukizwa Covid-19 mwezi uliopita lakini kwa bahati nilikuwa nimepata dozi mbili za chanjo, kwa hiyo hayakuwa na athari kubwa kwangu," alisema.

Aliwashauri Wakenya kuendelea kupata chanjo kwani chanjo imesaidia sana katika vita dhidi ya covid-19.

"Maambukizi ya pili yaliuwa watu wengi ikiwa ni pamoja na mwenyekiti wa muungano wangu na watu wengine wengi walikufa.

Maambukizi ya tatu ambayo yalianza kutoka India yalikuwa mabaya zaidi." Pia aliwashukuru wale waliokuja na chanjo.

Hii ni mara ya kwanza katibu huyo kufunguka na kufichua kwamba alipatikana na maambukizi ya corona.

Atwoli alisema virusi viko na lazima tujaribu daima na kuona jinsi tunaweza kuishi baada ya Covid-19.