Raila anapaswa kuondoa jam,Mudavadi amtaka Raila Odinga astaafu na kuwapa wengine nafasi

Muhtasari
  • Mudavadi alisema kuwa mnamo 2007 na 2017, alipuuza azma yake ya urais na kumpendelea Raila na Moses Wetang'ula wa Ford Kenya alifanya vivyo hivyo 2013

Kiongozi wa Amani National Congress Musalia Mudavadi kwa mara nyingine amemsuta kiongozi wa ODM Raila Odinga akimtaka kustaafu kutoka kwa siasa.

Akizungumza huko Butula, Kaunti ya Busia, Jumatatu, Mudavadi alisema Wakenya wamechoka na ni wakati wa waziri mkuu huyo wa zamani kutoa nafasi kwa watu wengine kuongoza.

Mudavadi alisema kuwa mnamo 2007 na 2017, alipuuza azma yake ya urais na kumpendelea Raila na Moses Wetang'ula wa Ford Kenya alifanya vivyo hivyo 2013.

“Tumechoka. Tunamwambia Raila aondoe jam watu wengine waende mbele,” Alisema Mudavadi.

Mudavadi alimtaja kinara wa chama cha Orange kama mradi wa serikali unaolazimishwa kwa Wakenya.

Kiongozi huyo wa ANC alimshutumu Rais Uhuru Kenyatta kwa kupanga kuingilia urithi wake licha ya kuwa amehudumu kwa mihula miwili kama mkuu wa nchi.

Alisisitiza kuwa wanachotaka ni heshima kutoka kwa rais.