Adhabu ya kifo Kenya, wakili Wajackoyah kuirejesha akiwa rais

Muhtasari

• Wajackoyah alisema kwamba pindi atakapochaguliwa kama rais, ataweka adhabu ya kifo kwa wale wote wanaoshiriki katika ufisadi na ubadhilifu wa pesa na mali za umma.

• Wajackoyah alisema kwamba wakenya wengi wanamsikiza na kumpenda kwa sababu anasema ukweli mtupu

George Wajackoya
George Wajackoya
Image: HISANI

Wakili George Wajackoyah ambaye pia ni mwaniaji wa urais katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9 amekuwa akigonga vichwa vya habari kwa manifesto yake tatanishi ambayo inawaacha wakenya wengi wakifikiria ni ndoto za alinacha.

Akizungumza katika mahojiano ya kipekee kwenye runinga ya KTN, Februari 16 usiku, Wajackoyah ameendelea kutoa maazimio na manifesto yake ikiwa atachaguliwa kama rais wa tano wa taifa la Kenya.

Alisema kwamba pindi atakapochaguliwa kama rais, ataweka adhabu ya kifo kwa wale wote wanaoshiriki ufisadi na ubadhirifu wa pesa na mali za umma.

“Adhabu ya kifo ndio njia pekee. Katika miaka mitano ya kwanza ya uongozi wangu, nitahakikisha hawa wabadhirifu wote wamehisi uchungu na ugumu wa maisha ambao wamewasababishia Wakenya ufujaji na wizi wa mali ya umma bila huruma,” alisema Wajackoyah

Wajackoyah alisema kwamba wakenya wengi wanamsikiza na kumpenda kwa sababu anasema ukweli mtupu na kusema kwamba chochote ambacho amekisema kwenye manifesto yake ni kweli na ndicho atawafanyia Wakenya.

Alitetea matamshi haya yake kwa kutolea mifano kwamba mataifa kama vile Phillipines, China, Singapore na baadhi ya mataifa kutoka Mashariki ya Kati ambayo yameendelea kiuchumi kwa adhabu kama hizi ambazo zinawaogofya wale wanaokuwa na fikira ya kuiba mali ya umma au kushiriki ufisadi.

Wakili huyo alisisitiza kwamba yeye si mtu wa itikadi kali bali anajaribu kusema ukweli na akasisitiza kwamba watuhumiwa wa ufisadi watapewa nafasi ya kukata rufaa dhidi ya kesi zao ila wakipoteza katika rufaa hizo, adhabu ya kifo itakuwa ni Rafiki wao namba moja.

“Kama utachukuliwa mahakamani, utakubaliwa kukata rufaa, ukipoteza unapewa adhabu ya kifo. Saudi Arabia na Urusi wanafanya hivo. Kuna ubaya wowote sisi pia tukienda njia hiyo ili kurejesha utimamu wa taifa?” aliuliza Wajackoyah

Katika manifesto yake, Wajackoyah alisema kwamba kuhalalisha uvutaji wa bangi ni moja kati ya maazimio yake atakayoyapa kipaumbele na akasema kwamba siku ataapishwa, atakuwa wa kwanza kuivuta mara ya kwanza na atakaribisha kila mtu kwenye ikulu ili waivute Pamoja.

Ajenda zingine kwenye manifesto ya wakili huyo mwenye utata ni kuhakikisha siku za kufanya kazi ni kutoka Jumatatu hadi Alhamisi, kinyume na ilivyo sasa Jumatatu hadi Ijumaa, Kuwaruhusu Waislamu muda Zaidi wa kuabudu siku za Ijumaa na kuhakikisha uchumi unaofanya kazi saa 24 kwa siku.