Viongozi wa Magharibi wakubaliana kusalia kwenye muungano wa Kenya Kwanza

Muhtasari
  • Viongozi wa Magharibi wakubaliana kusalia kwenye muungano wa Kenya Kwanza
Viongozi wa Magharibi wakubaliana kusalia kwenye muungano wa Kenya Kwanza
Image: Musalia Mudavadi/TWITTER

Viongozi wa eneo la Magharibi wakiongozwa na Kinara wa chama cha ANC Musalia Mudavadi na mwenzake wa FORD-K Moses Wetangula kwa kauli moja wamekubaliana kusalia kwenye muungano mpya wa Kenya Kwanza kama merikebu yao ya kusaka kule kubuni serikali ijayo ifikiapo Agosti 9 mwaka huu.

Kwenye mkutano wa viongozi hao uliowaleta Pamoja zaidi ya viongozi 6,000 waliokongamana katika eneo la Mululu, eneo bunge la Sabatia kaunti ya Vihiga, viongozi hao wamesema kuwa wako tayari kutembea safari ya kisiasa na naibu wa Rais William Ruto na hawana nia yeyote ya kuendeleza mazungumzo yeyote na upande wa Azimio la Umoja ambao wameutaja kuwa mradi wa wachache wanaojitakia makuu ya kisiasa na kibinafsi bila ya kuyajali maslahi ya wakenya na hasa wenyeji wa eneo kuu la magharibi mwa Kenya.

Mudavadi amesema kuwa mkutano wa leo ni msingi thabiti wa msukumo wa wenyeji wa eneo la magharibi mwa Kenya akisema kuwa sauti ya Pamoja waliozungumza nayo viongozi waliohudhuria mkutano wa leo ni hakikisho kuu la kuwa wenyeji wa eneo hilo wamechoka na kupotoshwa na baadhi ya viongozi wale waliowaunga mkono kisiasa kwenye siku za hapo awali.

Mudavadi pia akimsuta Rais Uhuru Kenyatta kuwajibika na kutangaza bayana ni maendeleo gani serikali yake ya Jubilee imewafanyia wenyeji wa eneo la Magharibi, huku akisema kuwa wao wamekataa  mradi wa Azimio ambao unanuia kuunga mkono Raila Odinga kama muwaniaji wa urais.

Viongozi wengine waliozungumza wakiongozwa na seneta wa kaunti ya Bungoma Moses Wetangula walisema kuwa jamii ya magharibi ambayo kwa sasa inajumuisha makabila mengine pasi tu na jamii ya abaluhya, kwamba wametumika sana kuwaunga mkono wengine huku wakitumika tu kama ngazi na hatimaye hawafaidi kwa lolote lile.

Kwenye maafikiano yaliyotokana na mkutano huo wa leo viongozi waliouhudhuria wamempa Musalia Mudavadi na Moses Wetangula uwezo, kibali na nguvu za kuzungumza na wandani wengine kisiasa huku wakiwataka kuhakikisha kuwa serikali ijayo wamo mpangoni kwenye kuibuni ili pia na wenyeji wa magharibi wanufaike.

Hali kadhalika, maafikiano hayo yamegusia umuhimu wa kuhakikisha kuwa kura za magharibi zinaingia kwenye kapu moja, wakisema kuwa viti vya maeneo bunge 39 eneo kuu la Magharibi vinyakuliwe na Kenya Kwanza, viti vyote vya ugavana, useneta na MCAs ili kuipa nguvu jamii ya magharibi kwenye meza ya mazungumzo ya kitaifa kwenye serikali mpya.