Ben Githae ni shahidi wangu--Moses Kuria atetea madai ya kuiba kura

Muhtasari
  • Matamshi hayo yalizua taharuki mitandaoni baada ya kuwaambia wajumbe kuwa yeye na watu wengine walisaidia kuiba kura kwa ajili ya Rais Uhuru Kenyatta
Moses Kuria
Image: Mercy Mumo

Mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria ametetea matamshi yake wakati wa Kongamano la Kitaifa la Wajumbe wa United Democratic Alliance (UDA) (NDC) lililoandaliwa katika uwanja wa Kasarani mnamo Jumanne.

Matamshi hayo yalizua taharuki mitandaoni baada ya kuwaambia wajumbe kuwa yeye na watu wengine walisaidia kuiba kura kwa ajili ya Rais Uhuru Kenyatta.

"Kuna wengine wanasema ati kura ya mlima itagawanywa; mheshimiwa Ann Waiguru, Rigathi Gachagua, Muthomi Njuki, Kimani Ichung’wa, Senator Linturi, Alice Wahome, Faith Gitau, Kimani wa Matangi…Sisi ndio tulikuwa tukishikilia Uhuru kura, na sisi ndio tulikuwa tunamuibia kura."

Lakini kulingana na mbunge anayewania kiti cha Ugavana wa Kiambu, wizi huo ulikuwa wa kuteleza tu.

Alichomaanisha, alieleza kupitia Facebook, ni kwamba yeye na mwimbaji wa nyimbo za Injili Ben Githae waliimba wimbo wa “Ndani ndani” wa kumpigia debe mkuu wa nchi.

“Ben Githae ni shahidi wangu. Tuliimbia Uhuru Ndani Ndani ya Ndani mpaka akashinda,” alifafanua mbunge huyo.

Madai ya wizi hivi majuzi yalimfanya Mwakilishi wa Mwanamke wa Murang’a Sabina Chege ajipate matatani na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Sabina aliambia umati katika Kaunti ya Vihiga kwamba kuna kitu kilifanyika kwa matokeo ya Raila Odinga 2017 na kwamba hali kama hiyo inaweza kuigwa katika uchaguzi wa mwaka huu.

Kesi ambayo inatazamiwa kuendelea kusikilizwa kikamilifu haikuweza kuanza mwezi uliopita baada ya kuugua.