Nitakubali matokeo ya kura huru na ya haki - Raila atangaza

Muhtasari
  • Akizungumza katika Chatham House London, Raila alisema atakubali matokeo ya kura ikiwa mchakato utakuwa huru na wa haki
Image: TWITTER// RAILA ODINGA

Aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga Jumatano alisema ataendelea tu na upande mzuri wa urithi wa Rais Uhuru Kenyatta hata akijitolea kukubali matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9 .

Akizungumza katika Chatham House London, Raila alisema atakubali matokeo ya kura ikiwa mchakato utakuwa huru na wa haki.

Kiongozi huyo wa ODM ambaye atakuwa akipeperusha bendera ya Azimio dhidi ya Naibu Rais William Ruto alisema tayari wamezungumza na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) wasiwasi wao kuhusu mchujo huru na wa haki.

"Imekuwa njia ndefu kufuatia chaguzi zisizo na tija za 2007, Wakenya walilipa bei kubwa sana na tulisema hilo halitafanyika tena," Raila alisema.

"Tumetaja maeneo ya wasiwasi tunayotaka (IEBC) kushughulikia ili kuhakikisha mchakato huo ni huru na wa haki."

"Ikiwa (uchaguzi wa rais) utakuwa huru na wa haki na tukashinda au kushindwa, tutakubali matokeo."

Wiki iliyopita, Ruto alikuwa na mkutano katika uwanja wa Thika kaunti ya Kiambu alimtaka Raila kujitolea hadharani kukubali matokeo ya uchaguzi na kutochukua hatua kali.

Kiongozi huyo wa upinzani pia alifafanua kuwa hataendeleza pande hasi za utawala wa Jubilee.

“Sijawahi kusema kwamba tutaendelea na mambo hasi. Tutaendelea na kazi chanya zinazofanywa na Rais Uhuru Kenyata,” akasema.

Mkuu huyo wa upinzani alitaja vita dhidi ya ufisadi kuwa baadhi ya mambo ambayo atafanya tofauti ikiwa atamrithi Rais Kenyatta.

Raila alisema mgawanyiko wa ndani katika utawala wa Jubilee umesambaratisha vita dhidi ya ufisadi akisema yeye habebi mizigo ya timu iliyogawanyika.

"Vita vyovyote dhidi ya ufisadi ni vya kisiasa, ikiwa mtu yeyote atachunguzwa kila mara kuna kilio hiki cha hivi na vile kinachunguzwa kwa sababu yeye ni mfuasi wangu," Raila alisema.

“Naingia pale nikiwa na mikono safi na watu wananifahamu. Sitakuja na huo mzigo.”

Raila pia aliunga mkono vuguvugu la Azimio La Umoja akieleza kuwa ni mwendelezo wa kupeana mkono na Rais Uhuru uliomaliza machafuko ya uchaguzi uliofuata uchaguzi wa urais wa 2017.

"Roho ya mazungumzo na hendisheki inaendelea katika Vuguvugu la Azimio La Umoja ambalo ninatafuta kuwa rais kwa tikiti yake," alisema.

Aidha alisisitiza haja ya marekebisho ya katiba ili kushughulikia baadhi ya maeneo yasiyofaa kwa utawala bora wa nchi.

Waziri Mkuu huyo wa zamani alisema Mpango wa Ujenzi wa Madaraja (BBI) ulikuwa pendekezo la kimaendeleo la kuboresha Katiba.

“Nina hakika kwamba Katiba yetu bado inahitaji marekebisho fulani. Kwa mfano, kuangalia kwa uwazi uhusiano kati ya Bunge na Watendaji ni wa dharura,” alisema.

Kiongozi huyo wa ODM pia alijitolea kukubali uamuzi wa Mahakama ya Juu kuhusu BBI.