Uganda yaipiku Kenya kwa watu wenye furaha zaidi duniani

Muhtasari

• Uganda inasimama katika nafasi ya 117 kote duniani wakifuatiwa na Kenya katika nafasi ya 119, Burundi wakiwa 137, Tanzania, 139 na Rwanda wakifunga orodha ya Afrika mashariki kwa kusimama nafasi ya 144.

Rais wa Kenya Uruhu Kenyatta na Mwenzake wa Uganda Yoweri Museveni
Rais wa Kenya Uruhu Kenyatta na Mwenzake wa Uganda Yoweri Museveni
Image: State House Kenya, Uganda

Wikendi iliyopita, shirika la World Happiness Report lilitoa orodha ya mataifa ambayo wananchi wake wako na furaha zaidi maishani.

Katika orodha hiyo ambayo imewashangaza wengi haswa nchini Kenya, mataifa mengi ya bara la Afrika watu hawana raha kabisa kutokana na kupanda kwa gharama ya kudumu mahitaji ya kawaida.

Finland inashikilia nafasi ya Kwanza kwa watu wenye furaha zaidi ambao wanahisi kama vile wanabarizi paradiso.

Inafuatiwa na mataifa ya Denmark, Switzerland, Iceland na Netherlands wanafunga orodha ya mataifa tano bora yenye watu wake wanaishi maisha ya furaha.

Barani Afrika, licha ya kukumbwa na msukosuko wa kiuchumi na vita vya wenyewe kwa wenyewe tangu kung’atuliwa kwa rais wao wa muda mrefu Muammar Gaddafi, taifa la Libya linaongoza kwa kushikilia nambari moja Afrika na nambari 78 kote ulimwenguni.

Ivory Coast wanashikilia nambari mbili Afrika (83) wakifuatiwa na Cameroon (89), Senegal (90) na Ghana (93) wakifunga tano bora kwa bara la Afrika.

Tukisongea nyumbani zaidi katika ukanda wa Afrika mashariki, taifa la Uganda liliorodheshwa kuwa na wananchi wenye furaha zaidi licha ya kuwa na matatizo ya uongozi ambapo rais wa muda mrefu Museveni anatajwa kuwa dikteta.

Taifa hilo linaorodheshwa kusimama katika nafasi ya 117 kote duniani wakifuatiwa na Kenya katika nafasi ya 119, Burundi wakiwa 137, Tanzania, 139 na Rwanda wakifunga orodha ya Afrika mashariki kwa kusimama nafasi ya 144.

Utafiti huu uliotolewa juzi umefanywa kwa muda usiopungua miaka mitatu iliyopita na shirika la tafiti hii lilisema lilizingatia vigezo mbalimbali ili kubaini mataifa yaliyo na watu wenye furaha na kisha kutoa orodha hiyo.

Baadhi ya vigezo vilivyozingatiwa ni pamoja na pato la taifa kwa kila mtu, usaidizi wa kijamii, umri wa kuishi kiafya, uhuru wa kuchagua maisha yako, ukarimu wa watu kwa ujumla, na mitazamo ya viwango vya rushwa ndani na nje.