Uhuru aomboleza Rais wa UAE Sheikh Khalifa Bin Zayed Al Nahyan

Muhtasari
  • Rais Kenyatta alimsifu marehemu Rais wa UAE kama kiongozi mwenye maono ambaye alibadilisha taifa hilo
Rais wa UAE Sheikh Khalifa Bin Zayed Al Nahyan

Rais Uhuru Kenyatta ametuma ujumbe wa rambirambi kwa Serikali na watu wa Umoja wa Falme za Kiarabu kufuatia kifo cha Rais Sheikh Khalifa bin Zayed Al Nahyan aliyeaga dunia siku ya Ijumaa akiwa na  umri wa miaka 73.

"Kwa niaba ya Serikali na Wananchi wa Kenya na kwa niaba yangu binafsi, napenda kuwasilisha rambirambi zetu kwa Serikali na Watu wa Umoja wa Falme za Kiarabu kufuatia kifo cha Rais Sheikh Khalifa bin Zayed Al Nahyan," Rais Kenyatta alisema katika ujumbe wake wa kufariji.

Rais Kenyatta alimsifu marehemu Rais wa UAE kama kiongozi mwenye maono ambaye alibadilisha taifa hilo la ghuba kuwa taifa kubwa kiuchumi.

"Mawazo na sala zetu ziko pamoja na familia yake, Serikali na watu wa Falme za Kiarabu wakati huu mgumu wa majonzi na msiba," Rais Kenyatta alisema.

Mkuu huyo wa Nchi alihakikisha kuwa Kenya imesimama kwa mshikamano na Serikali na watu wa Falme za Kiarabu na kuwaombea kwa Mwenyezi Mungu awafariji wanapoomboleza kiongozi wao aliyeondoka wa UAE.