DStv Kuongeza ada zake hadi 7.2% Kuanzia Septemba

Kampuni ya Multichoice inayomiliki DStv ilitangaza mapema Agosti kuongeza bei ya baadhi ya vifurushi na sasa kile cha Business kitapanda bei mwezi kesho

Muhtasari

• Gharama za juu zaidi zinakuja siku chache baada ya kampuni kurekebisha bei za wateja wa reja reja kutokana na kupanda kwa gharama za uendeshaji.

Kitanza mbali na kiwambo cha Multichoice, DStv
Kitanza mbali na kiwambo cha Multichoice, DStv
Image: The Star//Maktaba

Ni rasmi kwamba gharama ya maisha inazidi kupanda katika kila sekta ya maisha kutoka vyakula, kawi na kila kitu.

Gharama hiyo sasa imetambaa mpaka kugusa sekta ya burudani ambapo sehemu hizo kama migahawa, vinyozi, benki, kumbi za starehe na sehemu nyingine ambazo zinatumia huduma za DSTV zitalazimika kuingia mfukoni hata zaidi ili kupata huduma hizo.

Hii ni baada ya kampuni ya kampuni ya Multichoice inayomiliki DSTV kutangaza kuongeza vifurushi vyake vya biashara kwa hadi 7.2% kufuatia mfumuko wa uchumi kote ulimwenguni.

Kulingana na jarida moja la kibiashara la humu nchini, Kampuni hiyo ilitangaza Jumanne kuwa bei za juu zinazotumika kwa wateja wa kibiashara kwenye vifurushi vya DStv Business zitaanza kutumika kuanzia Septemba 1, 2022.

Gharama za juu zaidi zinakuja siku chache baada ya kampuni kurekebisha bei za wateja wa reja reja kutokana na kupanda kwa gharama za uendeshaji.

"MultiChoice Kenya ilirekebisha bei za usajili za vifurushi vyake vyote vya DStv katika notisi iliyotumwa kwa wateja mnamo Agosti 1, na pia itatumika kwa vifurushi vya DStv Business Work, Play na Stay," ilisema taarifa ya Multichoice kwa umma.

Kifurushi cha DStv Business Work kinafaa kwa shule, benki na ofisi za serikali, kifurushi cha DStv Stay kimeundwa mahsusi kwa ajili ya hoteli, hospitali na sehemu za makazi mbalimbali, huku DStv Play imeundwa kwa ajili ya migahawa, baa, vilabu na maduka.

Mnamo Julai mwaka jana, Multichoice iliboresha Biashara ya DStv kwa kutambulisha vifurushi vipya vya thamani ambavyo sasa vimejaa maudhui ya aina mahususi katika hatua iliyoongeza trafiki na hivyo mapato kwa makampuni ya biashara.

Taarifa hizi zinakuja huku ulimwengu ukiwa umekumbwa na mfumuko mbaya wa kiuchumi ambao baadhi ya wadadisi na wataalamu wa masuala ya kiuchumi wanasema hali hiyo imesababishwa na vita vinavyoendelea kati ya mataifa ya Urusi na Ukraine.

Nchini Uingereza, vyombo vya habari vilitangaza Jumatano asubuhi kwamba bei za bidhaa zimefumuka kwa ongezeko zaidi ya 10%, jambo ambalo halijawahi kutokea kwa zaidi ya miaka 48 iliyopita katika taifa hilo lenye ubabe kote duniani.

Benki ya Uingereza ilisema bei za bidhaa muhimu kama kawi, mkate, maziwa, mayai na nafaka ndizo zimeathirika zaidi.

“Benki ya Uingereza inasema ongezeko la hivi majuzi la bili za nishati, ambazo zimewekwa kuwa mara tatu zaidi ya ilivyokuwa mwaka mmoja uliopita, zitachochea mfumuko wa bei - kiwango cha kupanda kwa bei - hata juu zaidi, hadi 13%. Ongezeko la gharama za maisha linaweka finyu kwenye fedha za watu, kwani mishahara inashindwa kuendelea,” BBC iliripoti.