(+video) "Kilikuwa kifo cha ghafla" DCI yafutilia mbali uvumi Afisa wa IEBC Kirinyaga aliuawa

Hakuna mtu ameua mtu mwingine! - Afisa wa upelelezi wa jinai Laikipia alisema

Muhtasari

• “Nimesikia tetesi hata kwenye vyombo vya habari kuwa kuna mtu aliuawa. Waache wanaozungumza mambo kama hayo wakome,” Afisa huyo wa upelelezi alisema.

Msimamizi mkuu wa uchunguzi wa jinai katika kaunti ya Laikipia amejitokeza wazi na kupuuzilia mbali madai yanayoenezwa kweney mitandao ya kijamii kuhusu kifo cha ghafla cha afisa wa IEBC aliyekuwa akisimamia uchaguzi katika eneobunge la Gichugu kaunti ya Kirinyaga.

Usiku wa kuamkia Jumanne, kulikuwepo na taarifa za kifo cha afisa huyo wa IEBC aliyesemekana kuanguka chini ya kuzirai kabla ya kufariki na baadhi ya watu mitandaoni walianza kukihusisha kifo hicho na nguvu za mkono wa mtu , wengine wakisema kwamba huenda aliuawa  kutokana na sintofahamu ambayo imekuwa ikizingira maisha ya maafisa wa IEBC wiki moja baada ya mwili wa afisa mwingine wa tume hiyo aliyeuwa akisimamia uchaguzi eneobunge la Embakasi East kupatikana amefariki katika kichaka eneo la Loitoktok.

Afisa huyo msimamizi wa uchunguzi kaunti ya Laikipia katika video iliyopakiwa kwenye mtandao wa YouTube wa kituo kimoja cha runinga humu nchini alisikika akisema kweli ripoti ilifikishwa kituoni humo jana kwamab kuna mtu amezirai na kufariki alipokuwa akikimbizwa hospitali na kusisitiza kwamab hakuna mtu ameua mwingine na kwamba uchunguzi umeanzishwa pamoja na matokeo ya upasuaji wa mwili wake ndivyo pekee vitakuwa msema kweli na kuwataka wenye midomo waache kung’aka hovyo.

“Kesi hiyo iliripotiwa jana majira ya saa 2:38 usiku na taarifa ilikuwa ya kifo cha ghafla cha mtu aliyeanguka mjini (Nanyuki). Alikimbizwa hospitali ambapo alithibitishwa kuwa amefariki. Kwa hivyo hakuna mtu aliyeua mwingine. Hakuna kesi ya mauaji iliyoripotiwa hapa,” afisa huyo anaonekana akieleza kweney klipu hiyo.

Afisa huyo alitoa onyo kali dhidi ya watu ambao alisema kwamab amesikia hata kupitia vyombo vya habari vikisema kwamba kuna mtu ameuawa na kusema wanaosambaza taarifa za aina hiyo kukoma mara moja huku uchunguzi kamili ukisubiriwa kubaini kiini cha kifo cha afisa huyo wa IEBC.

“Nimesikia tetesi hata kwenye vyombo vya habari kuwa kuna mtu aliuawa. Waache wanaozungumza mambo kama hayo wakome,” Afisa huyo wa upelelezi alisema.

Taarifa za kifo cha afisa huyo kinafuata wiki mbili tu baada ya afisa mwenzake kutokweka na kisha mwili wake kupatikana jambo ambalo lilimlazimu mwenyekiti Wafula Chebukati kutangaza kusogezwa mbele kwa tarehe ya chaguzi zilizoahirishwa kutokana na sababu za kiusalama zinazowakumba maafisa wake wasimamizi wa uchaguzi.