Afisa wa IEBC aliyepatikana amefariki Loitokitok alikuwa na kisukari - Familia

Musyoka alitoweka mnamo Agosti 11 na mwili wake kupatikana Jumatano.

Muhtasari

•Muimi alisema kuwa kakake alikuwa na ugonjwa wa kisukari na kwamba madaktari walithibitisha kuwa tumbo lake lilikuwa tupu bila chembe ya chakula alipofariki.

•Madaktari walikubaliana kuchukua sampuli kumi na mbili kutoka kwa mwili wa Musyoka kwa ajili ya uchunguzi wa sumu na DNA jijini Nairobi.

Madaktari wa magonjwa wanajiandaa kuanza uchunguzi wa mwili wa Daniel Musyoka katika chumba cha kuhifadhi maiti cha hospitali ya Loitokitok siku ya Jumatano.
Madaktari wa magonjwa wanajiandaa kuanza uchunguzi wa mwili wa Daniel Musyoka katika chumba cha kuhifadhi maiti cha hospitali ya Loitokitok siku ya Jumatano.
Image: KURGAT MARINDANY

Mwanafamilia mmoja wa afisa wa IEBC wa Embakasi East aliyetoweka na mwili wake kugunduliwa Loitokitok mapema wiki hii amesema marehemu alikuwa na kisukari.

Jackson Muimi, kakake mdogo wa Daniel Musyoka, alisema kuwa kakake alikuwa na ugonjwa wa kisukari na kwamba madaktari walithibitisha Jumatano kuwa tumbo lake lilikuwa tupu bila chembe ya chakula alipofariki.

Hayo pia yalithibitishwa na kamanda wa polisi wa kaunti ndogo ya Kajiado Kusini Kiprop Ruto Ijumaa aliposema jamaa za Musyoka walikuwa wamethibitisha kuwa ana kisukari.

Mnamo Jumatano, madaktari watano walifanya uchunguzi wa maiti ya Musyoka, siku mbili baada ya mwili wake kupatikana na wafugaji kando ya mto kwenye mpaka wa Kenya/Tanzania, lakini matokeo yao kuhusu chanzo cha kifo chake hayakufahamika.

Madaktari wote watano walikubaliana kuchukua sampuli kumi na mbili kutoka kwa mwili wa Musyoka kwa ajili ya uchunguzi wa sumu na DNA jijini Nairobi.

Madaktari hao waliandamana na wataalamu wa uchunguzi wa CSI-DCI kutoka Nairobi, maafisa wa DCI kutoka Loitokitok, wawakilishi kutoka Haki Africa, IMLU, MedUp, IPOA, na familia.

Waliofanya uchunguzi wa maiti ni madaktari bingwa wa serikali; Dkt Dorothy Njeru, DR Richard Njoroge, na Dkt Titus Ngulungu.

Wengine kutoka sekta binafsi walikuwa; Dkt Omwok (aliyewakilisha IMLU), huku Dkt Edwin Walong akiwakilisha familia.

Musyoka alitoweka mnamo Agosti 11. Alikuwa katika kituo cha kuhesabia kura cha East Africa School of Aviation alipotoweka saa mwendo wa sasa nne kasorobo asubuhi.

Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati alisema walikuwa wamejaribu kumtafuta lakini hawakufanikiwa.

"Familia ya Musyoka na tume wamekuwa wakijaribu kumfikia bila mafanikio. Ripoti ya mtu aliyepotea imetolewa katika kituo cha polisi cha Embakasi," Chebukati alisema Jumatatu.

Daniel Musyoka's family members and relatives are in prayers at Loitokitok hospital mortuary on Wednesday.
Daniel Musyoka's family members and relatives are in prayers at Loitokitok hospital mortuary on Wednesday.
Image: KURGAT MARINDANY

Maswali yasiyo na majibu

Mkuu wa polisi wa Loitokitok, Ruto alisema Musyoka alihudumu kama afisa wa uchaguzi wa IEBC wa Kajiado Kusini hadi Mei, mwaka huu, alipohamishwa hadi Embakasi, Kaunti ya Nairobi, lakini hakuelewa sababu za waliomteka nyara hadi Loitokitok.

“Waliomleta kutoka Nairobi hadi hapa ni watu wanaoelewa eneo hili. Lakini tena, kama walitaka afe, kwa nini shida ya kumleta mpaka kwenye mpaka wa Kenya na Tanzania?” aliuliza Ruto.

Kwenye kipande cha kilomita 100 kutoka Emali, kwenye mpaka wa kaunti za Makueni na Kajiado, kuna vizuizi vitatu vya polisi kwenye barabara ya Loitokitock ambavyo vinasimamiwa saa 24/7.

Ruto na wanafamilia wa marehemu Musyoka wanaamini afisa huyo wa IEBC alipelekwa Loitokitok akiwa hai.

"Tulipopata mwili, ulikuwa mbichi ukiwa na alama ndogo tu kwenye mikono na miguu," Ruto alisema.

Muimi alisema walipoenda kutambua mwili wa marehemu kakake, ulikuwa mbichi na ilionekana kutupwa saa chache mapema.

"Kwetu sisi inaonekana hawakutaka kumuua kaka yangu, na tunashuku kwamba kwa sababu ya hali yake ya kiafya, ukosefu wa chakula na dawa kwa ugonjwa wake wa kisukari, aliaga dunia," alisema Mimi.

Familia bado haijapata ripoti kamili kutoka kwa madaktari waliochukua sampuli 12 kwa vipimo vya sumu na DNA.

Muimi alisema mwili huo utazikwa Agosti 26, nyumbani kaunti ya Thor Makueni.