•Kaimu IG wa Polisi Noor Gabow alishauri dhidi ya kukusanyika nje ya majengo ya mahakama katika mtaa wa Milimani, jijini Nairobi.
•"Maafisa wa polisi wa trafiki watatumwa vya kutosha ili kuelekeza trafiki kuzunguka kituo cha mahakama," Gabow alisema.
Image: DOUGLAS OKIDDY
Polisi wamewashauri Wakenya kufuatilia kesi wakiwa nyumbani wakati Mahakama ya Upeo itakapokuwa ikitoa uamuzi wake kuhusu kesi ya urais siku ya Jumatatu.
Katika taarifa yake Jumamosi, kaimu Inspekta Jenerali wa Polisi Noor Gabow alishauri dhidi ya kukusanyika nje ya majengo ya mahakama katika mtaa wa Milimani, jijini Nairobi.
"Tunataka kushauri umma kwa ujumla kuepuka kukusanyika katika Mahakama ya Upeo wakati wa uamuzi, au kuwa katika mikusanyiko ya watu lakini wafuate kesi kutoka kwa starehe ya nyumba zao," Gabow alisema.
Aidha, kaimu Inspekta Jenerali alisema maeneo ya mahakama yatadhibitiwa kwa matumizi ya umma na barabara zote zinazoelekea katika Mahakama ya Upeo zitafungwa.
"Maafisa wa polisi wa trafiki watatumwa vya kutosha ili kuelekeza trafiki kuzunguka kituo cha mahakama," alisema.
Mnamo Agosti 22, wafuasi wa Azimio la Umoja walizingira eneo la mahakama huku kiongozi wa muungano huo Raila Odinga akiwasilisha rufaa yake.
Wafuasi wa mwanasiasa huyo mkongwe walipiga kambi nje ya mahakama kwa saa kadhaa huku Raila na timu yake wakiwasilisha lori la ushahidi katika mahakama hiyo.
Siku ya Jumamosi timu ya Azimio ikiongozwa na bintiye Raila, Winnie Odinga ilikuwa imewaalika wafuasi wa muungano huo kwa maandamano ya amani kwenye vituo vya miji yote kwa heshima ya safari yao ya kutafuta haki. Jumbe hizo za mwaliko hata hivyo zilifutwa baadae kufuatia shinikiz la wanamitandao.
Mahakama itatoa uamuzi wake kuhusu kesi hiyo Jumatatu, Septemba 5, 2022 baada ya kukamilika kwa kusikilizwa kwa siku tatu siku ya Ijumaa.