(+video) Mbunge John Kiarie ataka Safaricom na M-Pesa kutenganishwa

Alisema kwamba ni wakati Safaricom isimamiwe na CA huku M-Pesa ikiwa chini ya CBK.

Muhtasari

• Mbunge huyo alikuwa akizungumza katika hafla ya kutambuishwa kwa wabunge wapya katika hoteli ya Safari Park jijini Nairobi.

Mbunge wa Dagoretti South na ambaye alikuwa mwigizaji wa ucheshi kwa muda mrefu John Kiarie sasa anataka kampuni ya mawasiliano ya Safaricom kushrutishwa kujitenga na kitengo cha mfumo wa upeperushaji pesa, M-Pesa.

Kiarie alisema kwamba itakuwa vizuri kwa vitengo hivyo viwili ambavyo kwa sasa vipo pamoja kama ulimi na mate kutenganishwa ili M-Pesa iwe chini ya mamlaka ya benki kuu ya Kenya, CBK huku Safaricom ikibaki chini ya mamlaka ya mawasiliano nchini, CA.

Akizungumza wakati wa mkutano wa kutambulishwa kwa wabunge wapya waliochaguliwa mnamo Jumanne, Septemba 20, katika Hoteli ya Safari Park jijini Nairobi, mbunge huyo wa UDA aliteta Safaricom na makampuni mengine ya mawasiliano yalikuwa yakifanya kazi kama benki.

“Tuna makampuni ambayo yamesajiliwa kama makampuni ya mawasiliano ambayo yanajiongeza maradufu kama benki. Kwa hali ilivyo sasa hivi, wanaanguka na kusimamiwa na Mamlaka ya Mawasiliano, lakini kwa sababu pia wanafanya miamala ya fedha, baadhi ya kanuni zinatoka CBK ambazo wanazitegemea,” Kiarie alisema.

Kiarie alipendekeza kwamba bunge hili la 13 linafaa kuingilia kati ili kupitisha mswada wa kuisaidia CBK kuchukua udhibiti wa mifumo yote ya miamala na makampuni ya mawasiliano yabaki tu kutoa huduma za mawasiliano kwa Wananchi.

“Je, bunge hili linaweza kusaidia vipi CBK katika kutunga sheria, na je, sheria hiyo ingemaanisha kwamba tutenganishe kampuni hizi za mawasiliano katika vitengo tofauti vya uendeshaji ambapo mawasiliano hujikita yenyewe yakidhibitiwa na CA, na kwenye vitengo vinavyotumia pesa vinavyodhibitiwa na CBK,” Kiarie aliongeza.