Msichana shujaa aliyeokoa wanafunzi 140 - Elgeyo Marakwet

Mavamizi hayo yalifanyika mnamo 17 Februari 2022 ambapo wavamizi walimiminia mabasi matatu ya shule.

Muhtasari

• Sylvia Cheptowot alikuwa kwenye mojawapo ya mabasi matatu yalioshambuliwa na kumwacha dereva mmoja kufariki.

Sylvia Cheptowot
Sylvia Cheptowot
Image: Youtube Screenshot

Huku Wakenya wakisherehekea sikukuu ya Mashujaa, wakazi wa eneo la Elgeyo Marakwet walimsherehekea msichana mdogo ambaye aliokoa wanafunzi 140 mikononi mwa maharamia wa Pokot.

Msichana huyu kwa jina Sylvia Cheptowot alikuwa kwenye mojawapo ya mabasi matatu ambayo majambazi walivamia mnamo 17 Februari 2022 walipokuwa wakirejea shuleni kutoka kwenye ziara ya elimu.

Siku hiyo  majambazi hao walifyatulia risasi basi la shule walimokuwa na kumuua dereva huku wakiwaacha wanafunzi kadhaa wakiwa wamejeruhiwa sana.

"Wanafunzi wenzangu walijeruhiwa. Mimi nilipigwa risasi miguu yote miwili, na mguu wangu mmoja ukavunjika," Msichana huyo alisema katika mahojiano na Citizen TV.

Licha ya kwamba alikuwa tayari ameumia na anavuja damu, mwanafunzi huyo wa shule ya upili ya Tot na mwenye umri wa miaka 16  aliambia wavamizi kwa lugha ya pokot kuwa:

 'Sisi ni wanafunzi kutoka Shule ya Upili ya Tot, msituue," 

Maneno hayo yenye ushujaa yaliwashawishi wavamizi hao na wakatoroka baada ya kugundua kuwa wanafunzi hao pia walikuwa kutoka Pokot. 

Tukio hilo hata hivyo lilimwacha na jeraha la mguu na sasa anatumia mikongongo. Majeraha yaliomfanya kukaa hospitalini kwa miezi mitatu na lililomfanya afanyiwe upasuaji kutoa risasi iliyokwama mguuni mwake.

Cheptowot alikuwa miongoni mwa mashujaa 230 wa kitaifa waliotambuliwa siku ya Mashujaa.