Serikali kutoa asilimia 90 ya huduma kwa njia ya dijitali

Ruto zaidi alisema hii itahusu ukusanyaji wa ushuru.

Muhtasari
  • Ruto alisema utoaji wa huduma za serikali kidijitali utahakikisha wakenya wanapokea huduma hizo hata wakiwa wamestarehe katika nyumba zao
DP RUTO WAKATI WA MANIFESTO YA KENYA KWANZA 30 JUNI 2022
Image: EZEKIEL AMING'A

Serikali inapanga kuhamishia huduma zake zote kwa mfumo wa kidijitali katika muda wa miezi 6-12 ijayo, Rais William Ruto ametangaza.

Ruto alisema ni asilimia 15 pekee ya huduma hizo zinazotolewa kwa sasa kidijitali huku juhudi za kufikia asilimia 90 zikiendelea.

"Ukiangalia manifesto yetu tulisema tutahamisha asilimia 80 ya huduma zote kwenye jukwaa la kidijitali na tunaifanyia kazi," alisema.

Ruto alisema utoaji wa huduma za serikali kidijitali utahakikisha wakenya wanapokea huduma hizo hata wakiwa wamestarehe katika nyumba zao.

"Tunataka kuhakikisha kuwa unaweza kupata kila huduma mtandaoni bila kusafiri hadi ofisi yoyote," alisema.

Rais Ruto alisema serikali pia itarahisisha utoaji wa huduma mbali mbali za serikali,  kama vile kuwawezesha wakenya kupata leseni zao kupitia kwa mtandao.

Ruto zaidi alisema hii itahusu ukusanyaji wa ushuru.

Naibu wake Rigathi Gachagua, Katibu wa Baraza la Mawaziri la Biashara Moses Kuria, rais wa KNCCI Richard Ngatia na mwenyekiti Kiprono Kittony walikuwa miongoni mwa waliohudhuria hafla hiyo.

Kittony alisema wamejitolea kuunga mkono utawala wa Kenya Kwanza kutekeleza ajenda yake.