Matiang'i aondoka makao makuu ya DCI baada ya kuhojiwa kwa saa kadhaa

Matiang'i alihojiwa na DCI kwa muda wa saa 8.

Muhtasari

• Viongozi wa Azimio akiwemo Eugene Wamalwa waliandamana naye katika makao makuu ya DCI.

Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani Fred Matiang'i akiwa nje ya makao makuu ya DCI Jumanne, Machi 7, 2023. Picha: ENOS TECHE
Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani Fred Matiang'i akiwa nje ya makao makuu ya DCI Jumanne, Machi 7, 2023. Picha: ENOS TECHE

Aliyekuwa waziri wa usalama wa ndani Dkt Fred Matiang'i hatimaye ameondoka makao makuu ya DCI baada ya kuhojiwa kwa muda wa saa nane.

Matiang'i alifika katika makao makuu ya DCI muda wa saa mbili  asubuhi siku ya Jumanne.

Hapo awali,kiongozi wa Azimio Raila Odinga aliwasili ili kuungana naye lakini alizuiliwa kuingia alipofika langoni.

 

Mawakili wa Matiang’i walikuwa wamesema kwamba mteja wao angewasili katika makao makuu ya DCI mwendo wa saa mbili, saa moja kabla ya muda aliyoelekezwa.

Wakili wake Danstan Omari alisema kwamba alimwandikia afisa wa mwaliko kumjulisha kuhusu mabadiliko hayo.

 

"Tunathibitisha kuwa tutakuwepo, hakuna chochote cha kuficha," alisema.

 

Matiang'i alikuwa anatakiwa kuhojiwa kuhusiana na madai ya polisi kuvamia nyumba yake huko Karen usiku wa Februari 8.

Polisi na idara zote za usalama walikanusha kuhusika na uvamizi huo wakidai kuwa uzushi.