Rais Ruto amuomboleza mbunge wa kwanza wa kike Kenya Mama Grace Onyango

Katika ujumbe wake wa rambirambi, Nyong’o alisema Kenya imepoteza kinara na nguzo kuu ya uongozi wa wanawake.

Muhtasari
  • Ruto alimsifu Mama Onyango kama mpiga debe ambaye alitekeleza jukumu muhimu kuchagiza maendeleo ya nchi
Mbunge wa kwanza wa kike Kenya Mama Grace Onyango
Image: TWITTER

Rais William Ruto aliongoza Wakenya kuomboleza Mama Grace Onyango, meya wa kwanza mwanamke wa Kisumu na mbunge wa kwanza mwanamke nchini Kenya.

Ruto alimsifu Mama Onyango kama mpiga debe ambaye alitekeleza jukumu muhimu kuchagiza maendeleo ya nchi.

“Rambirambi zangu kwa familia, marafiki na watu wa Kisumu kufuatia kufariki kwa Grace Onyango, meya wa kwanza mwanamke wa Kisumu na mbunge wa kwanza mwanamke nchini Kenya.

“Mama Grace alikuwa mvumbuzi ambaye alifungua milango ya ushiriki wa wanawake katika uongozi wa kisiasa. Alikuwa ni mwanamke shupavu, mzalendo wa hali ya juu na ujasiri usio na kigugumizi. Urithi wake utadumu kupitia kwa kila kiongozi wa kike aliyechaguliwa kwa vizazi vijavyo,”Aliongeza

Mama Grace, 98, alifariki alipokuwa akipokea matibabu katika Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Jaramogi Oginga Odinga (JOOTRH) mjini Kisumu Jumatano.

Gavana wa Kisumu Anyang Nyong’o, Seneta Tom Ojienda na Mbunge wa Kisumu ya Kati Joshua Oron pia wameomboleza Mama Onyango.

Katika ujumbe wake wa rambirambi, Nyong’o alisema Kenya imepoteza kinara na nguzo kuu ya uongozi wa wanawake.

“Mama Grace, almaarufu Nyarbungu, alikuwa mwenye umakini na mwenye maono. Mama na bibi kwa wengi.

"Mama na bibi kwa wengi, atakumbukwa kwa kuwashauri wasichana na viongozi wa kike," alisema.

Wiki iliyopita, gavana huyo alimtembelea nyumbani kwake Kisumu.