Wakongwe wa jeshi la Kenya wamteua Nelson Sechere kuwa Mkurugenzi Mtendaji

Shirika hilo linajumuisha na kuangazia watu ambao wamehudumu katika KDF na kustaafu au kujiuzulu.

Muhtasari

•KVP ilisema Bw Sechere atawaletea uzoefu mkubwa akiwa amehudumu katika mashirika mbalimbali ya umma.

•Lengo kuu la shirika hilo ni kuwaleta pamoja maveterani wa kijeshi wa KDF.

ameteuliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa KVP
Bw Nelson Sechere ameteuliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa KVP

Bw Nelson Sechere ameteuliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji mpya wa Maveterani wa Kenya kwa Amani  (KVP).

Katika taarifa iliyotolewa Machi 11, KVP ilisema Bw Sechere atawaletea uzoefu mkubwa akiwa amehudumu katika mashirika mbalimbali ya umma.

"Bw Sechere analeta uzoefu mkubwa baada ya kuhudumu kama mtaalam wa kukusanya fedha wa Umoja wa Afrika, pia ni Afisa Mkuu Mtendaji CHAE Kenya," taarifa hiyo ilisoma.

Bw Sechere pia anajulikana kwa kazi yake ya uhisani huku akitoa basi kwa Klabu ya Soka ya AFC Leopards mnamo Machi 2020.

Sasa amepewa jukumu la heshima la kuhudumu katika KVP, shirika ambalo lilianzishwa na kusajiliwa mwaka wa 2008 kufuatia makubaliano na idhini ya  Serikali.

Shirika hilo linajumuisha na kuangazia watu ambao wamehudumu katika KDF na kustaafu au kujiuzulu kwa sababu za huruma baada ya miaka mingi ya utumishi wa heshima.

Lengo kuu la shirika hilo ni kuwaleta pamoja maveterani wa kijeshi wa KDF, ili kutoa shukrani kwa jamii na kuipongeza serikali kwa ujenzi wa amani, usalama na maendeleo kwa kutumia uzoefu wao kama huduma ya kujitolea nje ya utumishi baada ya kustaafu.

Mwaka wa 2022, rais wa zamani Uhuru Kenyatta alitia saini na kufanya sheria mswada wa Maveterani wa KDF wa 2022 ambao kwa sasa unajulikana kama Sheria ya Mavetereni wa Majeshi ya Ulinzi ya Kenya ya 2022.