Polisi Wamuokoa mtoto wa siku nne aliyetupwa kwenye choo cha kanisa

Alikimbizwa katika Hospitali ya Marani Level 4 na kukabidhiwa kwa Afisa Mkuu Muuguzi wa Kaunti ndogo.

Muhtasari
  • Kwa msaada wa wananchi walibomoa shimo hilo la choo na kumchukua mtoto wa kike anayekadiriwa kuwa na umri wa siku nne na akionekana kuwa na afya njema.
Polisi Wamuokoa mtoto wa siku nne aliyetupwa kwenye choo cha kanisa
Image: NPS/TWITTER

Maafisa wa polisi kutoka Rioma, Kaunti ya Kisii wamemuokoa mtoto wa siku nne kutoka kwa choo cha shimo ndani ya boma la kanisa.

Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS) inasema mkaazi aliyehusika alisikia kilio cha mtoto mchanga kikitoka kwenye choo cha shimo ndani ya boma la Kanisa Katoliki la Rioma mnamo Jumanne, Aprili 18 na kuandikisha ripoti haraka katika Kituo cha Polisi cha Rioma.

"OCS na Maafisa kutoka kituo cha polisi walifika kwa haraka katika  eneo la tukio, takriban kilomita 1.4 kutoka kituoni," NPS inaongeza.

Kwa msaada wa wananchi walibomoa shimo hilo la choo na kumchukua mtoto wa kike anayekadiriwa kuwa na umri wa siku nne na akionekana kuwa na afya njema.

Alikimbizwa katika Hospitali ya Marani Level 4 na kukabidhiwa kwa Afisa Mkuu Muuguzi wa Kaunti ndogo.

NPS inasema mtoto huyo atachukuliwa na Kitengo chake maalum cha Ulinzi wa Mtoto.

"Tunampongeza mwananchi aliyetoa taarifa zilizofanikisha kuokolewa kwa mtoto kwa wakati, na tunamtakia mtoto wa kike, usalama na afya njema," mamlaka hiyo inaongeza.