Rais Ruto awaongoza Wakenya kumuomboleza mkewe Dedan Kimathi

Naibu Rais Rigathi Gachagua alitangaza serikali itamteua afisa mkuu atakayesimamia shughuli za mazishi.

Muhtasari
  • Mkuu wa nchi alisema Mama Mukami Kimathi alistahimili ukatili wa ukandamizaji wa wakoloni kwa ujasiri na alijivunia makovu ya vita.
Mjane wa shujaa wa Mau Mau Dedan Kimathi, Mukami Kimathi.
Mjane wa shujaa wa Mau Mau Dedan Kimathi, Mukami Kimathi.
Image: HISANI

Rais William Ruto amemuomboleza marehemu Mukami Kimathi, mke wa mpigania uhuru Dedan Kimathi.

Mkuu wa nchi alisema Mama Mukami Kimathi alistahimili ukatili wa ukandamizaji wa wakoloni kwa ujasiri na alijivunia makovu ya vita.

"Alivumilia hasara mbaya za vita kwa ujasiri wa kupendeza," alisema.

Kwa niaba yangu na ya familia yangu na kwa niaba ya watu wa Kenya, natuma ujumbe wa rambirambi kwa familia ya shujaa wetu aliyeaga, Mukami Kimathi."

Ruto alimtaja Mama Mukami kuwa mzalendo dhabiti na bingwa mashuhuri wa umoja wa kitaifa aliyewatia moyo Wakenya wengi wa rika zote kuenzi nchi yetu na kuwa tayari kutetea maadili yetu.

"Baada ya kushinda vita vya kupigania uhuru, Mama Mukami aliachwa nyuma kujilinda na kushinda mapambano ya kuwahudumia watoto wake bila kuwepo Field Marshall Kimathi. Kwa tabia yake, pia alishinda vita hivi," rais alisema.

"Ninaomba kwamba Mwenyezi Mungu akupe faraja yake ya kimungu wakati huu wa huzuni. Tutaheshimu kumbukumbu yake na kuthamini urithi wake. Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi."

Mukami Kimathi alifariki akiwa na umri wa miaka 96 alipokuwa akipokea matibabu katika hospitali moja jijini Nairobi baada ya kupata matatizo ya kupumua.

Aliaga dunia Alhamisi usiku.

Naibu Rais Rigathi Gachagua alitangaza serikali itamteua afisa mkuu atakayesimamia shughuli za mazishi.

Kulingana na bintiye Everlyn Kimathi Wangui, mama Mukami alifariki usiku wa kuamkia Ijumaa .

Mukami atakumbukwa sana kwa mchango wake wakati wa harakati za kupigania uhuru wa Kenya. Alikuwa miongoni mwa wanawake shujaa waliokuwa wakiwapelekea chakula wapiganaji wa Mau Mau wakiwa msituni.