Watoto wanaweza kuwa walidhulumiwa kingono huko Shakahola - Kindiki

Kindiki alisema kuwa walikua wanachunguza unyanyasaji wa kijinsia kwa watoto katika vibanda vilivyojengwa katika msitu huo wa ekari 800.

Muhtasari

• Alisema miongoni mwa mambo ambayo vyombo vya usalama vinachunguza, ni unyanyasaji wa kijinsia kwa watoto katika vibanda vilivyojengwa katika msitu huo wa ekari 800.

• Kufikia sasa, watu 39 wamekamatwa kuhusiana na mafundisho hayo ya mchungaji Mackenzie.

Waziri wa Usalama wa Ndani Kithure Kindiki akijibu maswali alipofika mbele ya Kamati ya Muda ya Seneti inayochunguza dhehebu la Shakahola Bungeni Ijumaa Mei 26,2023.
Waziri wa Usalama wa Ndani Kithure Kindiki akijibu maswali alipofika mbele ya Kamati ya Muda ya Seneti inayochunguza dhehebu la Shakahola Bungeni Ijumaa Mei 26,2023.
Image: EZEKIEL AMING'A

Waziri wa Usalama wa Ndani Kithure Kindiki amesema huenda watoto wa dhehebu la Shakahola walinyanyaswa wa kingono.

Alisema miongoni mwa mambo ambayo vyombo vya usalama vilikua vikichunguza, ni unyanyasaji wa kijinsia kwa watoto katika vibanda vilivyojengwa katika msitu huo wa ekari 800.

"Tuna baadhi ya njia ambazo mabanda hayo yanaweza kuwa yametumika pengine kwa tafrija za ngono zinazohusisha watoto," Kindiki alisema.

Akizungumza alipofika mbele ya Kamati ya Muda kuhusu Kuenea kwa Mashirika ya Kidini siku ya Ijumaa, Waziri huyo alisikitika kwamba huenda ukatili kama huo ulifanyika kwa kutumia jina la dini.

Alhamisi, Kindiki alitembelea kibanda cha mchungaji Paul Mackenzie katika msitu wa Shakahola ambapo inasemekana aliishi wakati wa kazi yake.

Mackenzie anashutumiwa kuwaongoza wafuasi wake kuamini kwamba ikiwa watakufa kwa njaa, watakutana na Yesu.

Kufikia Mei 25, miili 241 ilikuwa imefukuliwa kutoka kwa makaburi ya pamoja huko Shakahola.

Uchunguzi wa maiti 112 wa awali ulionyesha kuwa wengi wa waathiriwa walikufa kwa njaa huku wengine wakifa kwa kukosa hewa.

Daktari mkuu wa upasuaji wa maiti, Johansen Oduor alisema waathiriwa wakiwemo watoto walifariki kwa kunyongwa, kukosa hewa na kupigwa.

Kufikia sasa, watu 39 wamekamatwa kuhusiana na mafundisho hayo ya mchungaji Mackenzie.

Waliookolewa ni 91.

Siku ya Alhamisi, Kindiki alitangaza kuongezwa kwa marufuku ya kutotoka nje katika Ranchi ya Chakama.

"Hakutakuwa na harakati katika ranchi ya Chakama bila kibali cha Kamanda wa Kaunti ya Kilifi. Eneo hilo limesalia kuwa eneo la uhalifu na lisiloweza kufungwa na kila mtu isipokuwa maafisa wanaofanya kazi," Kindiki alisema.