Mwanamke aliyepigwa risasi wakati wa maandamano ya Saba Saba Kisii afariki

Familia ya Eunice Mutheu mwenye umri wa miaka 23 ambaye ni mwanafunzi wa chuo kikuu cha Kisii Polytechnic iko katika maombolezo

Muhtasari

• Mamlaka Huru ya Uangalizi wa Polisi inasema inachunguza ufyatuaji risasi na mengine mengi ambayo yaliripotiwa.

• Na huku maandamano mengine yakipangwa Jumatano, kuna mipango kutoka kwa viongozi wa eneo hilo na polisi kuhusu jinsi ya kushughulikia hali hiyo.

Mwanamke aliyepigwa risasi wakati wa maandamano ya saba saba huko Kisii afariki
Mwanamke aliyepigwa risasi wakati wa maandamano ya saba saba huko Kisii afariki
Image: Magati Obebo

Mwanamke mmoja alifariki kutokana na majeraha ya risasi aliyoyapata wakati wa maandamano ya Saba Saba katika Mji wa Kisii.

Familia ya Eunice Mutheu mwenye umri wa miaka 23 ambaye ni mwanafunzi wa chuo kikuu cha Kisii Polytechnic iko katika maombolezo. Inadaiwa alipigwa risasi na polisi.

Marehemu Eunice alifariki Jumamosi asubuhi kutokana na majeraha ya risasi aliyoyapata siku ya Ijumaa alipokuwa akisaidia biashara ya familia yake huko mjini.

Rafiki yake Mary Ngui alikuwa katika jengo moja na Eunice wakati wa maandamano.

“Tulikuwa watu watatu ndani ya nyumba hiyo na nilisikia kishindo kikubwa na kudhani ni kitoa machozi kilichogonga dirishani bila kujua ni Mary aliyepigwa. Baadhi ya risasi zimenasa ukutani,” alisema.

Jamaa zake wanasema alikuwa amerudi nyumbani kutoka chuo kikuu mwishoni mwa juma alipopatwa na mzozo.

Polisi wanasema waandamanaji hao walikuwa wanataka kuteketeza kituo cha polisi kabla ya kurudishwa nyuma na kusababisha mauaji hayo.

Gavana wa kaunti ya Kisii, Simba Arati alikashifu shambulizi hilo huku akitaka uchunguzi wa kina na wa haraka ufanywe kuhusu madai ya polisi kutumia risasi za moto wakati wa maandamano.

Anataka wanaopatikana na hatia kwa utovu wowote wa nidhamu wawajibishwe.

Kulikuwa na maandamano katika miji mikubwa nchini kuhusu gharama ya maisha.

Hii imewaacha wengine wanne wakiuguza majeraha hospitalini kufuatia maandamano hayo ambayo yaligeuka kuwa ghasia huku polisi wakiwakabili waandamanaji katika maeneo mbalimbali sehemu za mji.

Idadi ya watu waliouawa wakati wa maandamano nchini humo iliongezeka na kufikia watano baada ya kifo cha Eunice.

Vifo vingine viliripotiwa katika kaunti za Kisumu na Migori.

Mamlaka Huru ya Uangalizi wa Polisi inasema inachunguza ufyatuaji risasi na mengine mengi ambayo yaliripotiwa.

Na huku maandamano mengine yakipangwa Jumatano, kuna mipango kutoka kwa viongozi wa eneo hilo na polisi kuhusu jinsi ya kushughulikia hali hiyo.

Madereva na makondakta wa masafa marefu pia watagoma iwapo agizo la Mamlaka ya Kitaifa ya Uchukuzi na Usalama (NTSA) kuhusu kuwapima tena madereva halitaondolewa.

Maafisa wanatoa wito wa kufanyika kwa mazungumzo ili kuepusha mgomo huo kwa jumla.