Serikali ya Ruto yapendekeza ongezeko la ushuru wa VAT kutoka 16% hadi 18%

Pia hazina ya kitaifa ya fedha imependekeza tozo kwa huduma za mabwawa ya kuogelea shuleni, michezo ya tae kwondo, chess na skating – shughuli hizi zote shuleni zitakuwa zinatozwa ushuru wa VAT.

Muhtasari

• Mataifa mengine ya ukanda – Tanzania, Uganda, Rwanda, Burundi na Sudani Kusini yamesemekana kuwa yanatoza VAT kwa kiwango cha 18%.

Serikali kuongeza ushuru wa VAT.
Serikali kuongeza ushuru wa VAT.
Image: Maktaba

Wakenya watahitajika kukaza mikanda yao hata Zaidi kuelekea mbele huku serikali ikitoa pendekezo la kupandishwa kwa ushuru wa kukadiria ubora wa bidhaa, VAT kutoka kiwango cha sasa cha 16% hadi kiwango kipya cha 18%.

Kwa mujibu wa taarifa ya wizara ya fedha kama iivyochapishwa katika gazeti la The Star, pendekezo hilo linalenga kuwiana na ushuru wa VAT ambao mataifa wanachama wa Afrika Mashariki wanatoza bidhaa nchini mwao.

Kama pendekezo hili litapitishwa kuwa sheria, ina maana kwamba bei za bidhaa zitapanda mara dufu na hivyo kuwaweka Wakenya wengi ambao tayari wanaungulia machungu ya gharama ya juu ya maisha kuzidi kutaabika hata Zaidi.

Mataifa mengine ya ukanda – Tanzania, Uganda, Rwanda, Burundi na Sudani Kusini yamesemekana kuwa yanatoza VAT kwa kiwango cha 18%.

Ushuru wa VAT ambao hutozwa kila bidhaa iliyoko sokoni humu nchini ndio moja ya tozo zinazoingizia serikali ya Kenya hela nyingi za ushuru, kwani mamlaka ya ukusanyaji ushuru KRA iliongeza maokoto hayo kwa 5.23%, sawa na shilingi bilioni 27.34 mwaka jana hadi shilingi bilioni 550.04.

Kando na tozo hiyo, uongozi wa Ruto sasa hauachi chochote kupita bila kutozwa kwani wamependekeza pia kuelekeza macho yao katika baadhi ya huduma za kujivinjari shuleni ambazo hutolewa kwa wanafunzi na ambazo zinatajwa kutokuwa na uhusiano wa moja kwa moja na masomo.

Kwa mfano, hazina ya taifa ya hela imependekeza tozo kwa huduma za mabwawa ya kuogelea shuleni, michezo ya tae kwondo, chess na skating – shughuli hizi zote shuleni zitakuwa zinatozwa ushuru wa VAT.

“Baadhi ya shule zinatoa huduma ambazo hazina uhusiano wa moja kwa moja na masomo. Kuondolewa kwa ushuru wa VAT kwa huduma hizi huleta kutosawazishwa kwani baadhi ya huduma hizi zinapotolewa nje ya shule hutozwa ushuru,” sehemu ya pendekezo la hazina ya kitaifa ya pesa ilisoma.