Watu wa Nairobi hawakuli hizo ngumi mbwekse - Jaguar amsuta Sakaja kufukuza hawkers

“Na ninataka kumwambia Sakaja na ni rafiki yangu, kama wewe ni mwanamume kushinda Badi, gusa watu na wewe utaenda nyumbani,” Jaguar alisema.

Muhtasari

• Mimi nataka nimwambia gavana Sakaja, watu wa Nairobi hawakuli hizi ngumi unasema eti ngumi mbwekse.

• Siku mbili zilizopita, gavana Sakaja alitangaza ilani kwa wachuuzi wote wanaochuuza bidhaa zao katikati mwa jiji.

Jaguar amsuta Sakaja kuwafukuza wachuuzi Nairobi
Jaguar amsuta Sakaja kuwafukuza wachuuzi Nairobi
Image: Facebook

Aliyekuwa mbunge wa Starehe Charles Njagua Kanyi maarufu kwa jina la kisanii kama Jaguar amesuta na kupinga vikali hatua ya uongozi wa kaunti ya Nairobi kupiga marufuku wachuuzi wa bidhaa ndogo ndogo za kutembeza kutoka katikati mwa jiji la Nairobi.

Jaguar ambaye alikuwa anazungumza katika hafla wa wakfu wake wa Jaguar Youth Empowerment Foundation, alisema kwamba licha ya gavana wa Nairobi Johnson Sakaja kuwa rafiki yake wa karibu, lakini alisuta jinsi ambavyo mpango huo unafanywa, akisema kwamba watu wa kaunti hiyo ambayo ni kitovu cha uchumi wa Kenya hawali ngumi zake anazowaonesha hewani mbwekse.

“Juzi niliona gavana akisema eti hawkers hawatauzia town, mimi nataka nimwambia gavana Sakaja, watu wa Nairobi hawakuli hizi ngumi unasema eti ngumi mbwekse. Wale watu walikuchagua ni hawa, ukae chini na wao wajue vile watafanya kazi ndio waishi hizo nyumba unaishi za bei ya juu,” Jaguar alisema huku wafuasi wake wakimshangilia.

Jaguar ambaye alihudumu kwa kipindi kimoja tu bungeni alisema kwamba wakati wake kama mbunge, hakuwahi itikia hata mchuuzi mmoja kudhulumiwa, kwani katikati mwa jiji ni sehemu ya eneo bunge la Starehe.

“Mimi wakati nilikuwa mbunge na ninaweza kuapa hapa, sikuwa naitikia hawker hata mmoja kuguswa, na walikuwa wanafanya kazi na tunawachunga. Sisi tulizuia Jenerali Badi kufukuza hawkers, Sakaja ni nani awafukuze?” Jaguar alisema.

Msanii huyo alimalizia kwa kumchimba mkwara gavana Sakaja akimwambia kwamba ikiwa atawafukuza wachuuzi kutoka katikati ya jiji basi ajue ndio mwanzo anaanza kuandaa safari yake ya kwenda nyumbani katika uchaguzi mkuu wa 2027.

“Na ninataka kumwambia Sakaja na ni rafiki yangu, kama wewe ni mwanamume kushinda Badi, gusa watu na wewe utaenda nyumbani,” Jaguar alisema.

Siku mbili zilizopita, gavana Sakaja alitangaza ilani kwa wachuuzi wote wanaochuuza bidhaa zao katikati mwa jiji akisema kwamba wakati wao umekwisha na kuwataka wahame katika barabara zote za katikati ya jiji la Nairobi.